Nchi za Kiarabu zilizoiwekea vikwazo Qatar zadhurika kiuchumi
Kuongezeka mivutano katika uhusuano wa nchi nne za Kiarabu na Qatar kumezisababishia madhara makubwa ya kiuchumi nchi za Saudia na Imarati.
Imebainikwa kuwa, mzingiro wa pande zote uliowekwa na nchi hizo nne za Kiarabu dhidi ya Doha, si tu kuwa umesababisha matatizo kwa uchumi wa Qatar pekee, bali mzingiro huo pia umesababisha madhara kwa kwa soko la nchi nne zilizoiwekea vikwazo Qatar.
Wakati huo huo sambamba na Qatar kuwekewa vikwazo vilivyoanza yapata mwezi mmoja, baadhi ya makampuni ya kiuchumi duniani yenye makao yake Dubai katika Umoja wa Falme za Kiarabu yamepoteza karibu asilimia 10 ya masoko yake katika mwaka huu wa 2017.
Qatar ilikuwa ikidhaminia asilimia 80 ya mahitaji yake ya chakula na vifaa vya ujenzi kutoka Saudi Arabia na Imarati na sasa makampuni mengi ya nchi hizo mbili yameporomoka kiuchumi baada ya kufungwa mipaka baina ya nchi hizo na Qatar.
Gazeti moja linalochapishwa nchini Russia limeandika kuwa,Qatar inaweza kwa urahisi kutoa pigo kubwa kwa uchumi kwa Imarati kwa sababu nchi hiyo huagiza kutoka Qatar theluthi moja ya matumizi yake ya gesi ya kila siku. Aidha malori karibu 500 yaliyobeba bidhaa za kilimo za Saudi Arabia yamekwama kufuatia kufungwa mipaka ya nchi hiyo na Qatar na suala hilo limesababisha hasara ya zaidi ya dola milioni nane.