Saudia inahusika na kueneza virusi vya kipindupindu Yemen
Rais wa zamani wa Yemen, Ali Abdullah Saleh, amesema Saudi Arabia ndio chimbuko la mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu nchini Yemen ambao Umoja wa Mataifa umeutaja kuwa mbaya zaidi duniani.
Katika mahojiano na televisheni ya Roosiya Al Youm ya Russia, Saleh amesema muungano wa kijeshi unaongozwa na Saudia ndio unaohusika na kuenea ugonjwa hatari wa kipindipindu kwa kutumia silaha zilizopigwa marufuku kimataifa. Saleh ameongeza kuwa Saudi Arabia inatumia mabomu ya vishada na yale ya thermobaric dhidi ya raia wa Yemen na hivyo kusababisha madhara makubwa.
Aidha wataalamu wa tiba nchini Yemen wamefanya uchunguzi kuhusu ugonjwa wa kipindupindu ulioenea kote katika nchi hiyo na kubaini kuwa, Saudi Arabia imeeneza virusi vya uonjwa huo katika kile kinachohesabiwa kuwa ni vita vya kibiolojia dhidi ya Wayemen.
Idadi ya watu wanaougua kipindupindu nchini humo Yemen imepindukia 300,000 huku watu 1,600 wakiwa wameaga dunia tangu ugonjwa huo kuripotiwa mwezi Aprili.
Utawala wa Saudia ulianzisha mashambulizi ya kijeshi nchini Yemen mwezi Machi mwaka 2015 lengo likiwa ni kutaka kumrejesha madarakani kibaraka wake rais wa zamani wa nchi hiyo Abdu Rabbu Mansour Hadi.
Hadi hivi sasa mashambulizi hayo yameshaua na kujeruhi maelfu ya raia wa Yemen na kusababisha hasara kubwa kwa miundombinu ya nchi hiyo hasa mahospitali, mabwawa ya maji, shule, madaraja, misikiti n.k. Taasisi mbalimbali za kimataifa zimeitaja hatua ya Saudia na nchi waitifaki wake ya kuanzisha vita vya kivamizi huko Yemen kuwa ni jinai ya kivita.