Qatar: Ugaidi wa kisiasa ndio kikwazo cha vita dhidi ya ugaidi
Serikali ya Qatar imetangaza kuwa, ugaidi wa kisiasa na kifikra wa baadhi ya nchi za eneo la Mashariki ya Kati ndio kikwazo kikuu hii leo katika vita dhidi ya ugaidi.
Hayo yalielezwa na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Qatar katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Doha hapo jana Jumamosi akiwa pamoja na mgeni wake Jean-Yves Le Drian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ufaransa.
Mohammed bin Abdulrahman Al Thani amesisitiza juu ya udharura wa kuheshimiwa sheria za kimataifa na mamlaka ya mataifa kujitawala na kubainisha kwamba, katu vita dhidi ya ugaidi havitoweza kupata mafanikio kutokana na baadhi ya nchi kutanguliza mbele ugaidi wa kisiasa na kifikra.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Qatar amesema kuwa, hii leo vita dhidi ya ugaidi vinakabiliwa na vizingiti vingi ilhali panahitajika ushirikiano wa mataifa yote ili vita hivyo viwe na mafanikio.
Kwa upande wake, Jean-Yves Le Drian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ufaransa amesisitiza juu ya udharura wa kutatuliwa haraka mgogoro wa uhusiano baina ya nchi za Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi na kuonyesha wasiwasi alionao wa kuzidi kuwa mbaya hali ya Mashariki ya Kati.
Nchi za Saudia, Imarati, Bahrain na Misri zililikata mahusiano yao ya kila upande na Qatar tarehe tano Juni mwaka huu, na kuiwekea vikwazo vya kila upande vya baharini, nchi kavu na angani. Hata hivyo hadi sasa Qatar imekataa kusalimu amri mbele ya matakwa yasiyo na msingi ya Saudia na washirika wake.