Jul 25, 2017 07:54 UTC
  • Haider al-Abadi ataka kukomeshwa harakati zenye kuwagawa Wairaq

Waziri Mkuu wa Iraq, Haider al-Abadi, amewataka Wairaq wote na harakati za kisiasa za nchi hiyo kushikamana na kuwa na umoja na amepiga marufuku makundi yanayotoa nara zenye kulingania mgawanyiko na vitendo vya utumiaji mabavu.

Al-Abadi ameyasema hayo katika sherehe ya 'Wiki ya Ushindi wa Mosul' ambayo iliandaliwa na chama cha 'Daawa nchini Iraq ambapo pamoja na mambo mengine amevitaka vyama vya kisiasa kushiriki kwa namna iliyo bora katika uchaguzi ujao utakaofanyika mwezi Machi mwaka 2018.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Haider al-Abadi amezungumzia wajeshi wa Iraq na familia zao ambao wamejitolea katika mapambano dhidi ya ugaidi na kusema kuwa, serikali ya Iraq haitazembea katika kutimiza haki za mtu yeyote aliyejitolea katika kupambana na ugaidi nchini.

Jeshi la Iraq liliposhangilia ushindi wa Mosul

Akijibu ripoti zinazotolewa na baadhi ya mashirika ya kimataifa juu ya uwezekano wa kuwepo wahanga miongoni mwa raia wa kawaida katika operesheni ya kukomboa mji wa Mosul, Waziri Mkuu wa Iraq Haider al-Abadi ameyataka mashirika hayo ya kutetea haki za binaadamu kuchukua ripoti za kuaminika kutoka vyanzo vya kuaminika.

Waziri Mkuu wa Iraq alitangaza habari ya kukombolewa rasmi mji wa Mosul uliokuwa makao makuu ya kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) hapo tarehe 10 ya mwezi huu.

Tags