Qatar yakadhibisha madai mapya ya Saudi Arabia
Mkurugenzi wa Ofisi ya Mawasiliano ya serikali ya Qatar ameyataja madai mapya ya nchi nne za Kiarabu zilizoiwekea Doha vikwazo kuwa ni ya uwongo na yenye kukatisha tamaa.
Sheikh Hamad bin Salim Al Thani ameitaja orodha mpya iliyotolewa na Saudia na watifaki wake iliyowataja shakhsia na taasisi kadhaa zenye mfungamano na makundi ya kigaidi kuwa zinaungwa mkono na Qatar kuwa ni bandia. Hamad bin Salim Al Thani ameongeza kuwa nchi hizo badala ya kupambana na ugaidi zimeamua kuidhalilisha Qatar na kuharibu sura ya nchi hiyo.
Saudia, Imarati, Misri na Bahrain ambazo zimeiwekea Qatar vikwazo kwa kuituhumu kuwa inayaunga mkono makundi ya kigaidi, hivi karibuni zimechapisha orodha hiyo na kueleza kuwa taasisi na watu waliowekewa vikwazo wamekuwa na mahusiano ya moja kwa moja au kinyume chake na viongozi wa Qatar. Nchi hizo nne zimeziweka katika orodha yao mpya ya ugaidi taasisi tisa na shakhsia tisa waliodai kuwa na mahusiano na Qatar.