Jordan yamzuia balozi wa Israel kurejea mjini Amman
Serikali ya Jordan imeripotiwa kumzuia balozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel kurejea mjini Amman hadi pale hatua za kisheria zitakapochukuliwa dhidi ya mlinzi wa ubalozi wa Israel aliyeua raia wawili wa Jordan hivi karibuni.
Afisa wa ngazi ya juu wa serikali ya Jordan ambaye hakutaka jina lake litajwe ameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa, serikali ya nchi hiyo ya Kiarabu imemnyima kibali cha kurejea nchini Einat Schlein, balozi wa Israel mjini Amman hadi pale mlinzi wa ubalozi huo aliyefanya mauaji atakapofikishwa mbele ya vyombo vya sheria.
Juni 23 mlinzi huyo wa Kizayuni aliwaua raia wawili wa Jordan kwa kuwamiminia risasi, akiwemo kijana wa miaka 17 kwa jina Mohammed al-Jawawdeh, kwa madai kuwa walitaka kumshambulia.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, serikali ya Jordan na baada ya kufanya mazungumzo na viongozi wa Kizayuni, iliridhia kumuondoa nchini askari huyo wa Kizayuni aliyetambuliwa kwa jina Ziv Moyal, aliyehusika na mauaji hayo.
Kitendo hicho kilikosolewa vikali na asasi za kiraia, makundi ya kutetea haki za binadamu na Harakati ya Ikhwanul Muslimin ya Jordan zikisema kuwa hatua hiyo haikutosha.
Kadhalika maelfu ya raia wa taifa hilo walifanya maandamano makubwa wakitaka kufungwa kwa ubalozi wa Kizayuni mjini Amman na kuondoka mara moja balozi wake.
Aidha wabunge kadhaa waliamua kuondoka bungeni katika kulalamikia jinai hizo zilizofanywa na Israel na kuungwa mkono na serikali yao.