Senegal yapuuza ushawishi wa Saudia, sasa kumrejesha balozi wake nchini Qatar
(last modified Tue, 22 Aug 2017 08:13:01 GMT )
Aug 22, 2017 08:13 UTC
  • Senegal yapuuza ushawishi wa Saudia, sasa kumrejesha balozi wake nchini Qatar

Serikali ya Senegal imetangaza kuwa, itamrejesha balozi wake ambaye awali ilimwita nyumbani baada ya kuanza mgogoro kati ya nchi za Kiarabu za eneo la Ghuba ya Uajemi na Qatar.

Taarifa iliyotolewa na Ahmed bin Saeed Al Rumaihi, mkuu wa idara ya habari ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar imesema kuwa, baada ya Rais Macky Sall wa Senegal kufanya mazungumzo na Amiri wa Qatar, Tamim bin Hamad Al Thani, wamekubaliana kurejeshwa balozi wa taifa hilo la magharibi mwa Afrika mjini Doha.

Bendera za nchi zilizoiwekea vikwazo Qatar

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, katika mazungumzo hayo ya simu, Rais wa Senegal na amiri wa Qatar wamezungumzia masuala mbalimbali kuhusiana na kuinua kiwango cha mahusiano ya pande mbili.

Kurejea balozi wa Senegal nchini Qatar ni pigo kwa Saudia ambayo imekuwa ikifanya chini juu kuzishawishi nchi mbalimbali kuisusa Doha. Saudia, Imarat, Bahrain na Misri zilitangaza kukata mahusiano yao na Qatar mnamo tarehe tano Juni mwaka huu, hatua ambayo ilienda sambamba na kuliwekea vikwazo na mzingiro wa kila upande taifa hilo la Kiarabu. Mbali na mataifa hayo manne, nchi nyingine zikiwemo za Kiafrika kwa kufuata ushawishi wa Riyadh nazo ama zilikata au kupunguza mahusiano yao na Qatar.

Amiri Tamim bin Hamad Al Thani wa Qatar

Hii ni katika hali ambayo, usuluhishi wa kieneo na kimataifa kwa ajili ya kuhitimisha mgogoro huo, umeendelea kugonga mwamba huku kila upande ukiendelea kushikilia masimamo wake. Saudia na washirika wake, inaituhumu Qatar kuwa inaunga mkono makundi ya kigaidi, tuhuma ambazo zimekuwa zikikadhibishwa na serikali ya Doha.