Magaidi wa Daesh (ISIS) wajisalimisha kwa Hizbullah ya Lebanon
Wapiganaji wenye silaha wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) wamejisalimisha kwa vikosi vya muqawama baada ya vikosi hivyo kuwakaribia magaidi hao katika eneo la mpaka wa pamoja wa Lebanon na Syria.
Baada ya magaidi hao kujisalimisha kwa wapiganaji wa vikosi vya muqawama vya harakati ya Hizbullah walihamishiwa kwenye eneo la Deir ez-Zor mashariki mwa Syria.
Baadhi ya duru zimeripoti kuwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh limeipatia harakati ya Hizbullah taarifa kuhusu askari wa jeshi la Lebanon waliotekwa nyara na kundi hilo. Vikosi vya muqawama vitakabidhiwa viwiliwili vya mashahidi wanne waliozikwa kwenye eneo la Wadi Mira, huko Al-Qalamun nchini Syria. Kundi la kitakfiri la Daesh vilevile litamkabidhi kwa vikosi vya muqawama mateka mmoja pamoja viwiliwili vya mashahidi wengine wawili wa vikosi hivyo.
Wakati huohuo jeshi la Lebanon leo asubuhi limetangaza usitishaji vita katika maeneo ya Jarudul-qa'a na Ra's Ba'labayk katika mpaka wa pamoja wa nchi hiyo na Syria. Kamandi ya jeshi la Lebanon ambayo imeafiki kusitisha mapigano katika mpaka wa pamoja wa nchi hiyo na Syria kufuatia ombi la magaidi wa kundi la kitakfiri la Daesh limeeleza kupitia taarifa kwamba limechukua hatua hiyo kwa ajili ya kufanya mazungumzo kuhusu hatima ya wanajeshi wa Lebanon waliotekwa nyara na magaidi hao.
Makundi ya kigaidi na kitakfiri ambayo hivi karibuni yamelazimika kuondoka kwenye miinuko ya mji wa Arsal nchini Lebanon kufuatia operesheni za vikosi vya muqawama wa Kiislamu, miaka miwili nyuma yaliwaachia huru askari 16 wa Lebanon yaliokuwa yamewateka nyara, hata hivyo kuna askari wengine kadhaa wanaokadiriwa kufikia tisa ambao wangali wanashikiliwa mateka na makundi hayo.
Tarehe 19 ya mwezi huu wa Agosti, jeshi la Lebanon lilianzisha operesheni iliyopewa jina la Fajrul-Jurud dhidi ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh.../