Hamas yalaani shambulizi la anga la Israel nchini Syria
Harakati ya Mapambnao ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imelaani shambulio la Alkhamisi asubuhi la ndege za utawala wa Kizayuni wa Israel nchini Syria.
Mapema jana asubuhi, ndege za utawala wa Kizayuni zilishambulia kambi moja ya kijeshi ya Syria katika eneo la Misyaf kwenye viunga vya mkoa wa Hama na kuua wanajeshi wawili wa Syria na kuisababishia kambi hiyo hasara ya kiasi fulani
Hii si mara ya kwanza kwa ndege za Israel kushambulia maeneo ya wanajeshi wa Syria kwa lengo la kuwasaidia magaidi wanaozidi kuelemewa na mashambulizi ya jeshi la nchi hiyo.
Baada ya shambulio hilo la ndege za utawala wa Kizayuni, jeshi la Syria limeonya kuwa linahifadhi haki yake ya kulipiza kisasi cha damu za askari wake kama ambavyo pia limesema, mashambulio hayo ya Israel ni juhudi zisizo na maana za kujaribu kunyanyua mori na moyo wa magenge ya kigaidi yaliyoshindwa nchini Syria.
Mgogoro wa Syria ulianzishwa mwaka 2011 baada ya kuvamiwa na magaidi kutoka kona zote za dunia kwa uungaji mkono wa Saudi Arabia, Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel na waitifaki wao kama vile Uturuki kwa lengo la kuipindua serikali halali ya Rais Bashar al Assad.
Katika miezi ya hivi karibuni, askari wa serikali ya Syria kwa kushirikiana na askari wa mrengo wa muqawama wametoa pigo kubwa sana kwa magenge ya kigaidi yanayoungwa mkono na madola ya kigeni.