New York Times: Mgogoro wa Qatar umemshinda Trump
(last modified Sun, 10 Sep 2017 14:34:47 GMT )
Sep 10, 2017 14:34 UTC
  • New York Times: Mgogoro wa Qatar umemshinda Trump

Gazeti la New York Times la nchini Marekani limesema kuwa, rais wa nchi hiyo, Donald Trump ameshindwa kutatua mgogoro wa Qatar na nchi nne za Kiarabu zinazoongozwa na Saudia.

Gazeti hilo limegusia safari ya Amir wa Kuwait, Sabah Ahmad Jabir al Sabah, nchini Marekani, na mazungumzo ya simu ya rais wa Marekani Donald Trump na Amir wa Qatar pamoja na mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia na kuandika kuwa: Juhudi za Trump za kutatua mgogoro wa nchi hizo za Kiarabu kwa mazungumzo ya moja kwa moja baina ya Riyadh na Doha zimeshindwa kiasi kwamba Saudia imetangaza hadharani kuwa imesimamisha kikamilifu mazungumzo yake na Qatar.

Donald Trump akiwa katikati ya viongozi wa Kiarabu na Kiafrika mjini Riyadh, Saudi Arabia

 

New York Times limeongeza kuwa: Trump alizungumza kwa njia ya simu na Amir wa Qatar, Tamim bin Hamad Aal Thani na mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia, Mohammed bin Salman na kuwataka watatue mgogoro wao. Pamoja na hayo Saudia ilisema imesimamisha kikamilifu mazungumzo yake yote na Qatar.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, Mohammad bin Abdul Rahman Aal Thani alisema siku ya Ijumaa kuwa, nchi yake haiwezi kukubaliana na masharti 13 yaliyowekwa na Saudia na waitifaki wake kwani yanakwenda kinyume kikamilifu na haki ya kujitawala nchi hiyo.

Saudia, Imarati, Bahrain na Misri ziliiwekea vikwazo vya kila upande Qatar tarehe 5 Juni mwaka huu kwa madai kuwa Doha inaunga mkono ugaidi, inaingilia mambo ya ndani ya nchi hizo na haikubaliani na misimamo ya nchi hizo.

Tags