Misri: Kuna ulazima wa kutekeleza matakwa yaliyowasilishwa kwa Qatar
Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri amesema kuwa nchi nne zilizoiwekea vikwazo Qatar ziko tayari kutatua mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo.
Akizungumza mjini New York baada ya kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi nne zilizokata uhusiano na Qatar, Samih Shoukry amesema kuwa Imarati, Bahrain na Misri zipo tayari kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa wa Qatar iwapo Doha itajibu matakwa ya nchi hizo.
Shoukry ameongeza kuwa kikao kilichofanywa na nchi nne zilizoiwekea Qatar vikwazo kimesisitiza suala la mshikamano na kuheshimu matakwa yaliyowasilishwa kwa sababu jambo hilo lina udharura katika kulinda mamlaka ya kitaifa, uthabiti na maslahi ya nchi hizo nne.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri ameyatamka hayo huku Muhammad bin Abdulrahman Al Thani Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar akisema kuwa masharti yaliyotolewa na nchi zilizoiwekea Qatar vikwazo yanakiuka mamlaka ya kujitawala ya nchi hiyo.
Masharti makubwa yaliyoainishwa na Saudi Arabia kwa Qatar ni lile la kukata uhusiano wa kidiplomasia kati yake na Iran na harakati ya Hizbullah ya Lebanon, kufunga kikamilifu kanali ya al Jazeera na kuondoa kituo cha kijeshi cha Uturuki kilichoko huko Qatar. Saudi Arabia, Imarati, Bahrain na Misri tarehe Tano Juni mwaka huu zilitangaza kukata mahusiano yao ya kidiplomasia na Qatar zikiituhumu Doha kuwa inaunga mkono ugaidi na kwamba haiendi sambamba na malengo ya nchi hiyo. Baada ya kukata uhusiano huo wa kidiplomasia, nchi nne hizo za Kiarabu baadaye ziliiwekea Qatar mzingiro wa kiuchumi.