Hamas yaipongeza UN kwa kuiweka Israel katika orodha nyeusi
Harakari ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imepongeza hatua ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa ya kuiweka Israel katika orodha nyesi ya nchi zinazokiuka haki za binadamu.
Hamas pia imeitaka jamii ya kimataifa kuuchukulia hatua utawala haramu wa Israel kutokana na uhalifu na jinai unazoendelea kufanya dhidi ya watu wa Palestina.
Msemaji wa Hamas, Fauzi Barhum amesema uamuzi wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa ni hatua muhimu ya kudhihirisha hakika ya Israel kwa walimwengu na jinsi Wapalestina wanavyoendelea kukandamizwa.
Barhum amesema hatua hiyo inapasa kuwa mwanzo wa hatua nyingine za jamii ya kimataifa, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai na taasisi nyingine za kimataifa za kuiadhibu Israel na kutetea haki za Wapalestina zilizoghusubiwa.
Jumatano iliyopita Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa liliweka jina la utawala haramu wa Israel katika orodha nyeusi ya nchi na tawala 29 zinazokiuka haki za binadamu na kuwakandamiza watetezi wa haki hizo.