Mamia ya mamluki wa Saudia raia wa Sudan wauawa Yemen
Mkuu wa Kikosi cha Sudan kinachoshirikiana na muungano wa Saudi Arabia dhidi ya Yemen amesema mamia ya mamluki wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika wameuawa katika uvamizi wa muungano huo dhidi ya nchi hiyo maskini ya Kiarabu.
Mohammed Hamdan Hamidati ameliambia gazeti la Sudan la al-Jarida kwamba, mamluki 412 raia wa Sudan wameuawa kufikia sasa katika uvamizi huo wa muungano wa kijeshi wa Saudia dhidi ya jirani yake Yemen.
Hata hivyo, tovuti ya habari ya Yemenpress imeripoti kuwa, raia wa Sudan waliouawa katika uvamizi huo wa muungano wa Saudia nchini Yemen ni maradufu ya idadi hiyo iliyotajwa na Mkuu wa Kikosi cha Sudan.
Hivi karibuni, vikosi vya jeshi la Yemen vikishirikiana na vikosi vya kujitolea vya wananchi vilifanikiwa kuwaangamiza mamluki zaidi ya 80 wa Saudi Arabia katika wilaya ya Nimh, mkoani Sana'a.
Zaidi ya watu elfu 13 wa Yemen wameuawa kutokana na mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Saudia na washirika wake, tangu mwezi Machi mwaka 2015.
Lengo kuu la uvamizi huo wa muungano wa kijeshi wa Saudia dhidi ya Yemen ni kumrejesha madarakani kibaraka wao aliyekuwa rais wa nchi hiyo Abd Rabbuh Mansour Hadi.