Ismail Haniya: Hatutaweka chini silaha madamu wavamizi wangaliko ndani ya Palestina
(last modified Wed, 04 Oct 2017 02:22:18 GMT )
Oct 04, 2017 02:22 UTC
  • Ismail Haniya: Hatutaweka chini silaha madamu wavamizi wangaliko ndani ya Palestina

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema: madamu wavamizi wangaliko katika ardhi ya Palestina wananchi wetu wana haki ya kuwa na silaha.

Ismail Haniya ameyasema hayo katika mahojiano na kanali ya satalaiti ya ON Live ya  Misri ambapo mbali na kuashiria hatua zilizochukuliwa hivi karibuni na harakati ya Hamas za kuondoa hitilafu kati yake na harakati ya Fat'h na juhudi ilizofanya kwa ajili ya kufikiwa maridhiano ya kitaifa baina ya Wapalestina amebainisha kuwa: zama za hitilafu za ndani zimepita; na harakati ya Hamas imeshaamua kulipa gharama zozote zinazoilazimu kwa ajili ya kufanikisha maridhiano rasmi ya kitaifa.

Akijibu suali kuhusu silaha za muqawama, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas amesisitiza kuwa: madamu kuna uvamizi  ni haki ya wazi kabisa kuwa na muqawama na silaha kwa ajili ya kujihami; na hilo si jambo jipya.

Ismail Haniya (kulia) akihojiwa na kanali ya ON Live ya Misri

Ismail Haniya amefafanua kwamba harakati ya Hamas haiendeshi harakati nyengine zozote zile nje ya mipaka ya Palestina ikiwemo Misri na kwamba Hamas ni harakati ya ukombozi wa kitaifa ya Palestina inayoendesha harakati zake ndani ya mipaka ya Palestina. Ameongeza kuwa stratijia ya harakati hiyo ya muqawama wa Kiislamu ni kuwa na maelewano na uhusiano na nchi zote pasi na kuingilia masuala ya ndani ya nchi yoyote ile.

Matamshi ya Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas kuhusiana na haki ya harakati hiyo kuwa na silaha yametolewa katika hali ambayo Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel  amedai kuwa ikiwa tawi la kijeshi la Hamas katika Ukanda wa Gaza halitovunjwa hatoyatambua rasmi maridhiano yatakayofikiwa baina ya Wapalestina.../

Tags