Jeshi la Israel lashambulia ngome za Hamas Ukanda wa Gaza
Vikosi vya Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel vimeshambulia kile vinachodai kuwa ni ngome za Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas, katika Ukanda wa Gaza.
Habari zinasema vifaru vya jeshi katili la Israel vimeshambulia maeneo hayo usiku kucha, kwa madai kuwa linajibu mapigo baada ya eti Hamas kuvivurumishia roketi kutoka Gaza.
Hakuna ripoti yoyote ya majeruhi au vifo iliyotolewa na viongozi wa Palestina katika Ukanda wa Gaza kufikia sasa.
Hivi karibuni, Hamas ilitangaza kuwa, katu haitaweka kando muqawama na mapambano na kwamba, wanaotaka hilo lifanyike wanaota ndoto za alinacha.
Hii ni baada ya Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel, Benjamin Netanyahu kudai kuwa atayatambua maafikiano ya maridhiano ya kitaifa kati ya Hamas na Fat'h iwapo Hamas itavunja tawi lake la kijeshi.
Jeshi la utawala khabithi wa Israel limekuwa likitekeleza mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza, ambapo mara nyingi raia ndio wamekuwa wahanga wa hujuma hizo za kikatili.
Uvamizi wa Israel dhidi ya Gaza kuanzia Julai hadi Agosti mwaka 2014 ulipelekea Wapalestina 2,200 kuuawa shahidi huku wengine zaidi ya 11 elfu wakijeruhiwa.