HAMAS yasisitizia mapambano na Wazayuni ili kulinda matukufu ya Palestina
(last modified Tue, 10 Oct 2017 08:08:29 GMT )
Oct 10, 2017 08:08 UTC
  • HAMAS yasisitizia mapambano na Wazayuni ili kulinda matukufu ya Palestina

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imesisitiza kuwa suala la kupambana na Wazayuni maghasibu ambao wanayakalia kwa mabavu maeneo matakatifu ya Waislamu huko Palestina kama vile Masjidul Aqswa na Haram ya Nabii Ibrahim AS katika mji wa al Khalil wa kusini mwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, ni muhimu sana.

Ayman Abu Khalil, kiongozi wa ngazi za juu wa HAMAS amesema kuwa, kitendo cha wanajeshi wa Israel cha kuifunga Haram ya Nabii Ibrahim AS na kuwazuia Waislamu wa Palestina kusoma adhana na kusali ndani ya eneo hilo takatifu, ni uvunjaji wa wazi wa heshima ya matukufu ya Kiislamu.

Haram ya Nabii Ibrahim AS Palestina

 

Ameongeza kuwa, duru rasmi na wananchi wanapaswa kusimama imara kupinga uvamizi unaofanywa kila leo na walowezi wa Kizayuni ndani ya Msikiti wa al Aqsa na jinai ya Israel ya kupiga marufuku kusomwa adhana katika Haram ya Nabii Ibrahim AS.

Kiongozi huyo wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ameongeza kuwa, kuna wajibu kwa Waislamu kuweko muda wote katika maeneo hayo matakatifu ili kupunguza uvamizi na kuvunjiwa heshima na Wazayuni maeneo hayo matakatifu ya Waislamu.

Vile vile ameyataka makundi ya muqawama kutonyamazia kimya jinai hizo za wanajeshi wa utawala wa Kizayuni bali yanapaswa kukabiliana nazo kwa njia yoyote ile.

Hata jana Jumatatu wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel waliwazuia Waislamu kuingia katika Haram ya Nabii Ibrahim AS kama ambavyo pia waliwazuia kusoma adhana na kusali katika eneo hilo takatifu kwa madai ya eti sherehe za Mayahudi.

Tags