Hamas yasema mahasimu Palestina wafikia maelewano ya kitaifa
(last modified Thu, 12 Oct 2017 06:38:35 GMT )
Oct 12, 2017 06:38 UTC
  • Hamas yasema mahasimu Palestina wafikia maelewano ya kitaifa

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, imetangaza kufikia mapatano ya maelewano ya kitaifa na chama cha Fat'h kwa lengo la kuhitimisha mgogoro wa kisiasa wa muongo mmoja kuhusu utawala wa Ukanda wa Ghaza.

Kiongozi wa Hamas Ismail Haniyah amesema Alhamisi ya leo kuwa: "Fat'h na Hamas zimefikia mapatano mapema chini ya upatanishi wa Msiri."

Haniyah hakufafanua kuhusu mapatano hayo lakini afisa mwingine wa Hamas amesema maelezo zaidi yatatangazwa baadaye leo katika mkutano na waandishi habari.

Pande hasimu Palestina yaani Hamas na Fat'h (ambayo inafungamana na PLO)  Jumanne zilianza mazungumzo ya maelewano ya kitaifa huku kukiwa na matumaini kuwa kutapatikana muafaka baada ya mgogoro wa muda mrefu.

Maafisa wa pande zote wamesema mazungumzo hayo yameenda vizuri na kutapatikana natija kwa maslahi ya Wapalestina.

Hamas imekuwa ikiendesha serikali katika Ukanda wa Ghaza tokea mwaka 2006 wakati ilipopata ushindi katika uchaguzi wa bunge la

Kiongozi wa Hamas Ismail Haniyah

Palestina hatua ambayo ilimuacha Mahmoud Abbas wa chama cha Fat'h akiendesha mamlaka ya ndani ya Ukingo wa Magharibi.

Hamas sasa imeafiki kuvunja utawala wake Ghaza, kumkaribisha Abbas Ghaza na kukubali uchaguzi mpya ufanyike.

Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita Ghaza imekuwa chini ya mzingiro wa kinyama wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Aidha Ghaza imekumbwa na vita haribifu mara tatu kutoka utawala wa Kizayuni wa Israel. Hali katika eneo hilo lenye wakazi milioni 1.8  imefanywa kuwa mbaya kutokana na hatua za kiuhasama ambazo zimechukuliwa na Mamlaka ya Ndani ya Palestina inayosimamiwa na Abbas. Umoja wa Mataifa umetabiri kuwa iwapo hali ya sasa ya Ghaza itaendelea, eneo hilo litakuwa haliwezi kukalika tena ifikapo mwaka 2020.

Maelewano ya pande hasimu Palestina yatawawezesha Wapalestina kuelekeza nguvu zao zote katika kukabiliana na utawala haramu wa Israel.

 

Tags