Ripoti: Abbas asema hatochagua mawaziri kutoka HAMAS kama hawatokubali kuitambua Israel
Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ameripotiwa amesema kuwa hatowachagua wanachama wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS kuwa mawaziri katika serikali yake endapo hawatokuwa tayari kutamka wazi na hadharani kuwa wanautambua utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.
Gazeti la Kizayuni la Haretz limeripoti kuwa Mahmoud Abbas ametoa matamshi hayo katika mkutano aliofanya na wabunge wa zamani wa Israel waliomtembelea kwenye makao makuu ya chama chake cha Fat'h huko Ramallah, Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan hivi karibuni.
Mapema mwezi huu harakati ya Hamas ilisaini rasmi mkataba wa maridhiano ya kitaifa na harakati ya Fat'h kwa lengo la kuhitimisha mpasuko wa kisiasa wa karibu miaka kumi ambao chanzo chake kikuu ni suala la mamlaka ya uendeshaji eneo la Ukanda wa Gaza.
Makubaliano hayo yamemkasirisha Waziri Mkuu wa Utawala wa Kizayuni Benjamin Netanyahu, ambaye amesema Israel haitokubali maridhiano bandia ambapo upande wa Palestina ufikie maridhiano kwa gharama ya kuhatarisha uwepo wa Israel.
Mara baada ya kufikiwa makubaliano hayo, Netanyahu alitaka serikali mpya itakayoundwa ya umoja wa kitaifa ya Palestina iitambue Israe, ilivunje tawi la kijeshi la Hamas na kuvunja uhusiano na Iran.
Takwa hilo la utawala wa Kizayuni limetiliwa nguvu na Marekani ambayo imesisitizia dai la kuutambua utawala huo haramu na ghasibu.
Yahya Sinwar, kiongozi mwandamizi wa Hamas katika Ukanda wa Gaza amesema harakati yao haitokabidhi silaha zake, haitoitambua Israel wala haitovunja uhusiano wake na Iran. Akizungumza mapema mwezi huu Sinwar alisisitiza kwamba: "mjadala si juu tena ya kuitambua Israel, bali ni juu ya namna ya kuitokomeza".
Harakati za Hamas na Fat'h zimekuwa katika mzozo na mikwaruzano mikubwa tangu Hamas ilipopata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa bunge la Palestina uliofanyika mwaka 2006.
Tangu wakati huo, Hamas imekuwa ikishikilia hatamu za uendeshaji wa eneo la Ukanda wa Gaza huku mamlaka ya eneo la Ufukwe wa Magharibi yakiwa mikononi mwa harakati ya Fat'h.../