Hizbullah: Muqawama ndilo chaguo la pekee la Wapalestina
Afisa wa ngazi ya juu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema kuna haja ya kuendeleza mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel na kusisitiza kuwa Wapalestina hawana chaguo jingine ghairi ya muqawama.
Sheikh Naim Qassim, Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah aliyasema hayo jana Jumatano wakati wa kuanza kwa mkutano wa pili wa kimataifa wa Umoja wa Maulamaa wa Muqawama unaofanyika katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut.
Sheikh Qassim amebainisha kuwa, uhai wa Israel unategemea mauaji, uvamizi na ukaliaji wa mabavu sambamba na uungaji mkono wa jamii ya kimataifa akisisitiza kuwa, anatumai kuwa jitihada za muqawama karibuni hivi zitazaa matunda.
Kuhusu uwezekano wa utawala ghasibu wa Israel kufanya uvamizi mpya dhidi ya harakati hiyo ya muqwama nchini Lebanon, Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ameonya kuwa: Vituo vyote vya kijeshi vya utawala huo haramu vipo ndani ya shabaha ya makombora ya harakati hiyo.
Mkutano wa pili wa kimataifa wa Umoja wa Maulamaa wa Muqawama unahudhuriwa na shakhsia na maulamaa kutoka nchi zaidi ya 60 duniani, chini ya kaulimbu: Ahadi ya kweli, Palestina kati ya Tangazo la Balfour na Ahadi Takatifu.
Tangazo la Balfour lililoandikwa tarehe Pili Novemba mwaka 1917 na Waziri wa Mambo ya Nje wa wakati huo wa Uingereza Arthur James Balfour, lilikuwa chachu ya kuasisiwa utawala haramu wa Israel.