Wapalestina wakabiliana mara 290 na Wazayuni mwezi Oktoba 2017
Wapalestina wanaoishi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Quds tukufu wamekabiliana mara 290 na Wazayuni katika mwezi uliopita wa Oktoba.
Kwa mujibu wa kituo cha upashaji habari cha Palestina, makabiliano hayo yamejumuisha mashambulizi na uvamizi uliofanywa na Wazayuni dhidi ya Wapalestina.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, katika mwezi uliopita wa Oktoba, wanamapambano 12 wa Palestina kutoka harakati za Jihadul Islami na HAMAS wameuawa shahidi.
Kituo hicho kimeongeza kuwa, katika mwezi uliopita, kumetokea kesi 290 za makabiliano baina ya Wapalestina na Wazayuni maghasibu ambapo Wapalestina 75 na Wazayuni 16 wamejeruhiwa. Mzayuni mmoja ameangamizwa katika kipindi hicho.
Wakati huo huo katika mwezi uliopita, wanajeshi Wazayuni wamewafyatulia risasi mara 70 wakulima na wavuvi wa Kipalestina katika Ukanda wa Ghaza na kuwateka nyara Wapalestina 500 katika meneo tofauti ya Ukingo wa Magharibi na Baytul Muqaddas.
Intifadha ya Quds ya wananchi wanamuqawama wa Palestina ilianza mwezi Oktoba 2015 kwa ajili ya kupambana na jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel. Zaidi ya Wapaelstina 380 wameshauawa shahidi wakiwemo watoto wadogo 96 tangu ilipoanza Intifadha hiyo hadi hivi sasa.