Rais wa Lebanon akataa ombi la kujiuzulu Hariri, amtaka arejee nchini
Rais Michel Aoun wa Lebanon amesema atakubali ombi la Waziri Mkuu wa nchi hiyo Saad Hariri la kujiuzulu kwa sharti kiongozi huyo aliyeko Saudi Arabia kwa sasa arejee nchini na atoe ufafanuzi wa kina.
Vyanzo vya habari kutoka Kasri ya Rais wa Lebanon vimedokeza kuwa, Rais Aoun hadi sasa hajakubali ombi hilo la Hariri tangu walipowasiliana kwa njia ya simu hapo jana, na kwamba amemtaka mwanzo arejee nchini na ampe maelezo ya kina yaliyompelekea ajiuzulu.
Hariri alitangaza kujiuzulu siku ya Jumamosi akiwa mjini Riyadh, katika taarifa aliyotoa kwa njia ya televisheni, akitaja sababu kadhaa zilizomfanya achukue uamuzi huo wa ghafla. Hariri alidai kuwa, miongoni mwa sababu hizo ni hali ya usalama ndani ya Lebanon, na kwamba anahisi kuna njama ya kutaka kumuua.
Hali kadhalika Hariri ameituhumu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa inaingilia masuala ya nchi za Kiarabu za eneo ikiwemo Lebanon na kuongeza kwamba Hizbullah ni nguzo ya Iran katika eneo.
Hata hivyo Iran kupitia Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Bahram Qassemi imesema kujiuzulu Saad Hariri wadhifa wa uwaziri mkuu wa Lebanon ni ishara ya hila mpya inayofanywa ili kuzusha mivutano ndani ya Lebanon na eneo la Mashariki ya Kati.