Hariri ajidhalilisha Saudia, apanga foleni kumpa mkono Mfalme Salman
Kanda ya video iliyorushwa hewani na televisheni ya utawala wa Aal-Saud imemuonyesha Waziri Mkuu wa Lebanon aliyetangaza kujiuzulu hivi karibuni akijidhalilisha kwa kupanga foleni na maafisa wa serikali ya Riyadh kwa ajili ya kumpa mkono Mfalme Salman Bin AbdulAzizi wa Saudi Arabia.
Video hiyo imeonyesha namna Hariri alivyojishushia hadhi kwa kusimama kwenye mstari akiwa pamoja na maafisa wa utawala wa Riyadh kwa ajili ya kuinama na kuubusu mkono wa Mfalme Salman, ambaye alikuwa ametoka mji mtukufu wa Madina.
Wakati huo huo, Rais Michel Aoun wa Lebanon amesisitiza kuwa, sharti watawala wa Riyadh watoe ufafanuzi kuhusu 'kumteka nyara' Saad Hariri na ni kwa nini wanaendelea kumzuilia hadi sasa.
Hii ni katika hali ambayo, hivi karibuni chama cha al-Mustaqbal kinachoongozwa na Saad Hariri, kimesema kuwa bado kinamtambua kuwa ni waziri mkuu wa Lebanon huku kikimtaka arejee nyumbani kwa ajili ya kuweka mambo sawa nchini humo.
Viongozi wa Lebanon wameikosoa vikali Saudia kwa kuingilia masuala yake ya ndani na kuchochea migogoro ya kisiasa nchini humo.
Jumamosi iliyopita, chini ya mashinikizo Saad Hariri akiwa mjini Riyadh alitangaza kujiuzulu wadhifa wake wa uwaziri mkuu wa Lebanon; na masaa machache baadaye Saudia na Kuwait zikawataka raia wao waondoke mara moja nchini Lebanon.