Saudia ipo tayari 'kuitoa kafara' Palestina ili kuimarisha uhusiano na Israel
Mshauri wa zamani wa Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel amesema utawala wa Aal-Saud wa Saudi Arabia uko tayari 'kuitoa kafara' Palestina kwa lengo la kuimarisha uhusiano wake na Tel Aviv.
Gazeti la The Telegraph limemnukuu Yaacov Nagel, aliyekuwa Mshauri wa Masuala ya Usalama wa Netanyahu ambaye alitangaza kujiuzulu wadhifa wake mapema mwaka huu akisema kuwa, Riyadh ipo tayari kufanya chochote ili kurejesha uhusiano wake na Israel katika hali ya kawaida.
Amesema watawala wa Riyadh kwa sasa wanajishughulisha zaidi na namna ya kuboresha uhusiano wao na Tel Aviv, na wala hawajali chochote kuhusu makubaliano ya amani yatakayofikiwa kati ya Israel na Palestina.
Kauli hii inajiri siku chache baada ya Yuval Steinitz, Waziri wa Nishati wa Israel kufichua kuwa, utawala wa haramu wa Israel una uhusiano wa kificho na nchi nyingi za Kiarabu.
Licha ya Misri na Jordan kuwa ndio nchi pekee za Kiarabu zenye uhusiano wa kidiplomasia na utawala wa Kizayuni wa Israel, lakini watawala wa Israel wamekuwa wakiongea wazi wazi kuhusu uhusiano wao na nchi za Kiarabu.
Novemba 18, Avigdor Liberman, Waziri wa Vita wa Israel aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa: Wakati umefika kwa Eneo la Mashariki ya Kati kuunda muungano dhidi ya Iran.