Hamas: Silaha zetu ni mstari mwekundu, hazina mjadala
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, imepinga mwito wa kuitaka iweke chini silaha kama sehemu ya maridhiano ya kitaifa kati yake na harakati ya Fat'h.
Khalil al-Hayya, afisa mwandamizi wa Hamas amesema katika kikao na waandishi wa habari mjini Gaza kuwa, suala la silaha za harakati hiyo ni mstari mwekundu na wala haliwezi kufanyiwa mjadala.
Amesema ni haki ya harakati hiyo kuendelea kupambana na uvamizi na kukaliwa kwa mabavu wa ardhi za Palestina unaofanywa na utawala ghasibu wa Israel hadi jitihada zao zizae matunda.
Khalil al-Hayya ameongeza kuwa, harakati ya muqawama ya Hamas itaendelea na njia yake ya kutafuta maridhiano ya kitaifa na kundi hasimu la Fat'h kwa maslahi ya Wapalestina.
Mwezi Oktoba mwaka huu, Hamas ilitangaza kufikia mapatano ya maelewano ya kitaifa na chama cha Fat'h chini ya upatanishi wa Misri, kwa lengo la kuhitimisha mgogoro wa kisiasa wa muongo mmoja kuhusu utawala wa Ukanda wa Gaza.
Harakati mbili hizo zimekuwa katika msuguano tangu mwaka 2006, baada ya Hamas kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa bunge.