Maandamano Bahrain kulaani utawala unaomdhulumu Sheikh Isa Qassim
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i37101-maandamano_bahrain_kulaani_utawala_unaomdhulumu_sheikh_isa_qassim
Maandamano mapya ya wananchi yameripotiwa kote Bahrain kwa lengo la kulaani utawala wa kiimla wa ukoo wa Aal Khalifa ambao unamdhulumu na kumnyima matibabu mwanazuoni maarufu wa Kiislamu Ayatullah Sheikh Isa Qassim.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 03, 2017 02:45 UTC
  • Maandamano Bahrain kulaani utawala unaomdhulumu Sheikh Isa Qassim

Maandamano mapya ya wananchi yameripotiwa kote Bahrain kwa lengo la kulaani utawala wa kiimla wa ukoo wa Aal Khalifa ambao unamdhulumu na kumnyima matibabu mwanazuoni maarufu wa Kiislamu Ayatullah Sheikh Isa Qassim.

Taarifa zinasema maandamano yamefanyika Jumamosi katika eneo la Sanabis nje ya mji mkuu Manama ambapo wananchi waliokuwa na hasira walikusanyika katika mitaa ya Abu Sabi na Maqsha. Waandamanaji walikuwa na mabango yaliyoandikwa , 'Ghadhabu ya Mapinduzi' huku wakilaani utawala wa kifalme wa ukoo wa Aal Khalifa.

Watu wanne walikamatwa Ijumaa wakiwa katika maandamano ya amani ya kulaani utawala wa Aal Khalifa ambao umemfunga kifungo cha nyumbani Sheikh Isa Qassim kwa muda wa  karibu siku 500.

Maandamano hayo yanajiri wakati Umoja wa Ulaya umeelezea wasiwasi wake kutokana na hali mbaya ya kiafya  ya Sheikh Issa Qassim, aliyezingirwa kila upande na askari wa utawala wa Aal Khalifa.

Umoja wa Ulaya umesema unafuatilia kwa karibu hali mbaya ya kiafya ya Sheikh Issa Qassim nchini Bahrain.

Maandamano ya kutaka Sheikh Isa Qassim aachiliwe huru

Tamko hilo la Umoja wa Ulaya limesema, hatua zilizochukuliwa na serikali ya Bahrain dhidi ya Sheikh Issa Qassim zinakinzana na nasaha zilizotolewa na kamati huru ya kutafuta ukweli nchini humo na kwamba Umoja wa Ulaya unapendekeza kufanyika mabadiliko makubwa ya kimsingi nchini Bahrain kwa ajili ya kurejesha umoja wa kitaifa na utulivu.

Kuanzia tarehe 14 Februari 2011, wananchi wanamapinduzi wa Bahrain walianzisha wimbi la kupinga utawala wa kiimla wa nchi hiyo na kutaka haki zao za kimsingi kama za kujichagulia wenyewe viongozi wao. Hata hivyo Saudi Arabia ilituma jeshi lake na kukandamiza maandamano ya amani ya wananchi wa nchi hiyo, ingawa jeshi hilo la Aal Saudi limeshindwa kuzima harakati hizo za wananchi wa Bahrain.