Russia: Magaidi wameshaangamizwa kikamilifu Syria
Mkuu wa Jeshi la Russia ametangaza kuwa, vikosi vyote vya genge la kigaidi la Daesh (ISIS) vimeangamizwa nchini Syria na kwamba nchi hiyo ya Kiarabu imesafishwa kikamilifu na uwepo wa magaidi.
Shirika la habari la Itar Tass la Russia limemnukuu Jenerali Valery Gerasimov akitangaza rasmi habari hiyo jana na kusisitiza kuwa, ardhi yote ya Syria imesafishwa na uwepo wa magaidi na kwamba vikosi vya nchi hiyo hivi sasa vinadhibiti maeneo yote ya nchi.
Mkuu huyo wa jeshi la Russia ameongeza kuwa, jeshi la Syria lilifanikiwa hivi karibuni kuangamiza pote la mwisho la kundi la kigaidi la ISIS katika mji wa Deir ez-Zor mashariki mwa Syria.
Jenerali Gerasimov ameulaumu muungano wa Marekani nchini Syria na kusema kuwa, muungano huo unadai kupambana na magaidi nchini Syria lakini mji pekee uliokombolewa na muungano huo huko Syria ni Raqqa ambao kimsingi haukukombolewa bali umeangamizwa na kuteketezwa na Wamarekani na waitifaki wake na hivi sasa Raqqa imefutika katika ramani ya dunia, imekuwa ni mahame ambayo watu hawawezi tena kuishi.
Tangu miaka miwili iliyopita, Russia iliingia katika vita vya kupambana na magaidi nchini Syria kwa ombi rasmi la serikali halali ya nchi hiyo ya Rais Bashar al Assad.
Tangu miaka sita iliyopita, kundi la nchi za Kiarabu na za Magharibi maadui wa Syria zikiongozwa na Marekani ziliivamia kila upande nchi hiyo ya Kiarabu kwa lengo la kupindua serikali ya Rais Bashar al Assad. Nchi hizo zilimimina magaidi nchini Syria kutoka kila kona ya dunia na kuwapa mafunzo ya kijeshi, silaha na fedha nyingi lakini licha ya kufanya jinai zisizofikirika, zimeshindwa katika njama zao nchini humo.