Marekani yaionya Saudia dhidi ya mienendo yake Mashariki ya Kati
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i37375-marekani_yaionya_saudia_dhidi_ya_mienendo_yake_mashariki_ya_kati
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani ameitahadharisha Saudi Arabia juu ya matokeo mabaya ya vitendo vyake katika eneo la Mashariki ya Kati.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 09, 2017 07:23 UTC
  • Marekani yaionya Saudia dhidi ya mienendo yake Mashariki ya Kati

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani ameitahadharisha Saudi Arabia juu ya matokeo mabaya ya vitendo vyake katika eneo la Mashariki ya Kati.

Rex Tillerson aliyasema hayo jana Ijumaa katika safari fupi aliyoifanya Paris, mji mkuu wa Ufaransa na kuongeza kuwa, Riyadh inapaswa kutafakari juu ya mienendo yake dhidi ya Yemen, Qatar na majirani zake wengine katika eneo la Mashariki ya Kati.

Amesema: "Kuhusu namna viongozi wa Saudia wanavyoamiliana na Qatar, namna wanavyoshughulikia vita dhidi ya Yemen na mgogoro wa Lebanon, tunawashauri wawe makini na watafakari sana kuhusu taathira hasi za vitendo vyao."

Kadhalika hapo jana, Ikulu ya White House ya Marekani iliutaka utawala wa Aal-Saud uruhusu kufikishwa misaada ya kibinadamu kwa raia wa Yemen kupitia bandari ya Hudaidah na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Sana'a.

Trump na mkewe wakiondoka Riyadh baada ya kusaini makubaliano ya mauzo ya silaha

Hii ni katika hali ambayo, Marekani imekuwa ikiiunga mkono Saudia katika vita vyake dhidi ya Yemen kwa kuipa msaada wa kiintelijensia, kilojistiki, na kuizia silaha zenye thamani ya mabilioni ya dola.

Mapema mwezi Mei, Rais Donald Trump wa Marekani alisaini makubaliano ya kuiuzia Riyadh silaha zenye thamani ya dola bilioni 350 za Marekani.