Sisitizo la kudumishwa mapambano ya Intifadha huko Palestina
Maelfu ya wananchi wa Palestina jana Alkhamisi walikusanyika katika Medani ya al Katiba katika eneo la Ukanda wa Gaza wakipiga nara na kaulimbiu ya "Mapambano ni Uamuzi Wetu, na Umoja ni Chaguo Letu" na kuadhimisha mwaka wa 30 tangu kuasisiwa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS).
Mkuu wa Idara ya Siasa ya Hamas, Ismail Haniya ambaye amehutubia mkusanyiko huo amesema kuwa, hakati ya Hamas ni mwendelezo wa mapambano ya ukombozi na kusimama kidete katika ardhi ya Palestina. Kwa hakika Hamas na Intifadha ni harakati mpya katika njia ya Wapalestina ya kupigania haki zao na kukabiliana na njama za aina mbalimbali za utawala wa Kizayuni wa Israel na muungaji mkono wake mkuu yaani Marekani.

Matukio ya sasa ya Palestina yameonesha kuwa, nchi hiyo na Quds tukufu ndio kadhia nambari moja ya Umma wa Kiislamu, na Ulimwengu wa Kiislamu unalifuatilia suala hilo kwa umakini mkubwa. Hapo mwaka 1987 wakati ilipoanza Intifadha ya Kwanza Wapalestina walianzisha harakati za Hamas na Jihad Islami wakijibu ukandamizaji uliokuwa ukifanywa na utawala wa Kizayuni na kuonesha kuwa, wana azma imara na kubwa ya kudumishwa mapambano ya ukombozi. Tangu wakati huo kulipandikizwa mbegu za muqawana na mapambano mapya dhidi ya Wazayuni maghasibu na washirika wao. Kuanzishwa kwa harakati hizo za mapambano ya ukombozi za wananchi kulivuruga kabisa mahesabu ya utawala ghasibu wa Israel. Muda mfupi baada ya kuanzishwa Intifadha ya Kwanza nchi za Magharibi zinazouunga mkono utawala haramu wa Isarel zilianzisha kile kilichopewa jina na mwenendo wa mapatano ya Mashariki ya Kati ili kuzima na kufubaza harakati ya mapambano. Hata hivyo kuwa macho kwa harakati hizo za mapambano na makundi ya wananchi kumezuia njama hiyo na kuifanya butu.

Katika mkondo huo huo huo, mjumbe wa ngazi ya juu wa harakati ya Jihad Islami, Khalid al Batsh anasema: "Mahudhurio makubwa ya Wapalestina katika maadhimisho ya mwaka wa 30 tangu kuasisiwa harakati ya Hamas ni aina fulani ya kura ya maoni na kura ya "ndio" kwa chaguo la mapambano, muqawama na jihadi." Al Batsh ameongeza kuwa: "Mahudhurio hayo makubwa ya wananchi ni sawa na ngumi ya chuma dhidi ya uamuzi wa Rais wa Marekani, Donald Trump, wa kuitambua Quds tukufu kuwa ni mji mkuu wa Israel."
Kupamba moto kwa mapambano ya Intifadha baada ya kuundwa harakati za Hamas na Jihad Islami kulikwamisha kivitendo harakati za Israel za kutaka kuimarisha zaidi misingi ya utawala huo ghasibu katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina na kuipa kadhia ya Palestina sura ya kimataifa. Harakati hizo pia zimethibitisha kwa mara nyingine kwamba, mapambano ndiyo njia bora zaidi ya kukomboa Palestina na kurejesha haki zilizoghusibiwa za wakazi asili wa nchi hiyo. Harakati ya Intifadha iliweka utaratibu mpya wa mapambano dhidi ya utawala haramu.

Alaa kulli hal, kutokana na mafanikio ya Hamas na harakati nyingine zinazoamini kuwa mapambano ndiyo njia pekee ya kukomboa ardhi ya Palestina, na kushindwa mtawalia kwa utawala huo haramu katika medani mbalimbali za kisiasa na kijeshi katika miaka ya hivi karibuni, Wapalestina waliowengi wanaamini kuwa, njia pekee ya kurejesha haki zao na kupigania matukufu yao ni kudumishwa mapambano na kuendelea kusimama kidete dhidi ya Wazayuni maghasibu. Imani hiyo imeimarika zaidi baada ya kubainika athari mbaya za mwenendo wa mazungumzo eti ya amani ya Mashariki ya Kati yanayosimamiwa na Marekani.