Haniya: Quds ni Mji Mkuu wa Palestina na Waislamu wote
Kiongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, amesema kuwa, "Quds Tukuf (Jerusalem) ni mji mmoja usioweza kugawanywa pande mbili za Mashariki na Magharibi na ni mji mkuu wa Wapalaestina na Waislamu wote."
Ismail Haniya aliyasema hayo Jumanne katika hafla iliyofanyika kusini mwa Ukanda wa Ghaza na kuongeza kuwa: "Taifa la Palestina halijashangazwa na kura ya turufu (veto) ya Marekani katika Baraza la Usalama kwani hatua hiyo ni katika fremu ya sera kuu za Marekani ambayo ni muitifaki mkuu wa na wa daima wa utawala wa Kizayuni wa Israel."
Jumatatu, licha ya wanachama 14 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuupigia kura ya ndio muswada uliopendekezwa na Misri kuhusu mji mtakatifu wa Quds, lakini Marekani imeukwamisha muswada huo kwa kura yake ya veto. Tarehe sita mwezi huu wa Disemba, rais wa Marekani, Donald Trump kwa mara nyingine tena aliwavuruga walimwengu kwa kitendo chake cha kiuadui cha kuitangaza Quds Tukufu kuwa eti ni mji mkuu wa utawala pandikizi wa Kizayuni.
Ismail Haniya amesisitiza kuwa, Hamas inapinga uamuzi wa Trump kuhusu Quds Tukufu huku akisema kuna ulazima wa kuchukuliwa hatua za kubatilisha uamuzi huo.
Kiongozi wa Hamas pia ametoa wito wa kuwepo umoja miongoni mwa nchi za Kiarabu katika Ghuba ya Uajemi huku akizitaka ziweke kando hitilafu zao na kusuluhisha matatizo kupitua mazungumzo na kuheshimiana.
Ismail Haniya ametaka nchi za Kiarabu zitenge fedha kwa ajili ya kuunga mkono mji wa Quds na kuwasaidia Wapalestina wanaoishi katika mji huo ambao kimsingi ni watetezi wa Msikiti wa al Aqsa, kibla cha kwanza cha Waislamu.