Mahmoud Abbas: Wapalestina hawatokubali tena mpango wowote wa Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i37953-mahmoud_abbas_wapalestina_hawatokubali_tena_mpango_wowote_wa_marekani
Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema taifa lake "halitokubali tena" mpango wowote wa Marekani kwa ajili ya kile kinachoelezwa kama mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati na kuiita nchi hiyo "mpatanishi asiye na mwamana".
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 22, 2017 23:13 UTC
  • Mahmoud Abbas: Wapalestina hawatokubali tena mpango wowote wa Marekani

Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema taifa lake "halitokubali tena" mpango wowote wa Marekani kwa ajili ya kile kinachoelezwa kama mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati na kuiita nchi hiyo "mpatanishi asiye na mwamana".

Abbas aliyasema hayo mbele ya waandishi wa habari baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa huko mjini Paris hapo jana.

Amesema, Marekani imethibitisha kuwa ni mpatanishi asiyeaminika katika mchakato wa amani na kwamba Wapalestina hawatokubali tena mpango wowote utakaopendekezwa na Washington.

Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina aidha amelaani kitisho kilichotolewa na Rais Donald Trump wa Marekani cha kukata misaada ya kifedha kwa nchi zilizopiga kura katika Umoja wa Mataifa dhidi ya hatua ya Washington ya kuitambua Quds kuwa mji mkuu wa Israel.

Mahmoud Abbas (kulia) alipokutana na Donald Trump, huko Ramallah, Palestina

Katika mkutano huo na waandishi wa habari, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa naye pia alikosoa vikali uamuzi wa Marekani wa kuitangaza Quds kuwa mji mkuu wa Israel na kusema: "Wamarekani wamejitenga wenyewe; na mimi nitajitahidi nisifanye kitu kama hicho".

Hata hivyo Rais wa Ufaransa alisema hatochukua mapema hatua ya upande mmoja ya kulitambua dola la Palestina na kusisitiza kwamba Paris itachukua uamuzi huo "katika wakati mwafaka".

Macron aidha ametangaza kuwa atafanya safari katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina katika mwaka ujao wa 2018.

Siku ya Alkhamisi,  Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliulaani kwa wingi mkubwa wa kura uamuzi wa rais Donald Trump wa Marekani wa kuitangaza Baitul Muqaddas kuwa mji mkuu wa Israel. Katika upigaji kura wa kihistoria, nchi 128 wanachama wa Umoja wa Mataifa walilipigia kura za 'ndiyo' azimio hilo la Quds, wanachama wanane tu ikiwemo Marekani na utawala haramu wa Israel zilipiga kura za 'la' na nchi nyengine 21 ziliamua kutopiga kura.../