Ripoti: Israel inashikilia miili 766 ya Wapalestina tangu Oktoba 2023
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i136202-ripoti_israel_inashikilia_miili_766_ya_wapalestina_tangu_oktoba_2023
Mamlaka za Israel zinashikilia miili ya Wapalestina 766 waliokwishatambuliwa, huku karibu nusu ya miili hiyo ikishikiliwa tangu Oktoba 2023, wakati Israel ilipoanzisha vita vya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza ulio chini ya mzingiro.
(last modified 2026-02-03T09:36:48+00:00 )
Feb 03, 2026 07:56 UTC
  • Israel inashikilia mamia ya maiti za Wapalestiina
    Israel inashikilia mamia ya maiti za Wapalestiina

Mamlaka za Israel zinashikilia miili ya Wapalestina 766 waliokwishatambuliwa, huku karibu nusu ya miili hiyo ikishikiliwa tangu Oktoba 2023, wakati Israel ilipoanzisha vita vya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza ulio chini ya mzingiro.

Gazeti la Haaretz linalochapishwa katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) limeripoti kuwa miili 520 ya Wapalestina imehifadhiwa katika mochwari za kijeshi za utawala wa Kizayuni na mingine 256 iliyosalia imewekwa katika makaburi yenye namba maalumu. 

Ripoti ya Haaretz imeeleza kuwa miili isiyopungua 373 ya Wapalestina ilipelekwa katika seli za Israel baada ya Oktoba7, 2023. 

Aghalabu ya raia hao wa Palestina waliuawa na wanajeshi wa Israel  na 88 walikuwa mateka ambao walipoteza maisha katika mazingira magumu wakiwa katika magereza ya Israel miaka miwili iliyopita.

Aghalabu ya mateka hao wa Kipalestina waliaga dunia wakiwa kizuizini baada ya kushikiliwa na utawala wa Kizayuni bila ya kufunguliwa mashtaka. 

Ripoti zinaonyesha kuwa idadi isiyojulikana ya miili ya Wapalestina ya kuanzia mwaka 1967 na miaka iliyofuata, ilizuiliwa na kuzikwa katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.

Zaidi ya hayo, Israel pia inashikilia miili 10 ya raia wa kigeni.