HAMAS: Intifadha itaendelea hadi malengo ya Wapalestina yafikiwe
Kiongozi mwandamizi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema Intifadha ya Quds itaendelea hadi malengo ya Wapalestina yafikiwe.
Mushir al-Masri amesema muaqwama wa Palestina umepata mafanikio katika kukabiliana na jinai za Israel na kusisitiza kuwa harakati ya muqawama itaendelea hadi malengo ya Wapalestina yatakapofikiwa ikiwemo kuhitimisha kukaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina na utawala wa Kizayuni.
Kiongozi huyo mwandamizi wa Hamas ametilia mkazo pia kudumishwa umoja baina ya Wapalestina na kueleza kwamba taifa la Palestina linapaswa kuwa kitu kimoja katika kukabiliana na adui Mzayuni.
Aidha ameutaka umma wa Kiislamu uendelee kushikamana na malengo ya Palestina likiwa ndilo suala kuu la Ulimwengu wa Kiislamu na kusisitiza juu ya kustawishwa uhusiano wa Hamas na nchi zote za Kiarabu na za Kiislamu.
Wakati huohuo mahakama moja ya utawala wa Kizayuni wa Israel imetoa kibali kwa walowezi wa Kizayuni kuvamia nyumba za Wapalestina.
Mahakama hiyo ilitoa hukumu hiyo jana Ijumaa kwa walowezi hao pamoja na shirika moja lenye mfungamano nao liitwalo Ilad, ambayo inawapa kibali cha kuvamia nyumba za Wapalestina na kuwanyang'anya mali na milki zao.
Kwa muda sasa walowezi wa Kizayuni wanaoishi kwenye eneo la Silwan, Baitul Muqaddas Mashariki wamekuwa wakitaka kuvamia nyumba za Wapalestina na kupora milki zao lakini mahakama moja ya Israel ikazuia jambo hilo.../