Bahrain, kisiwa kilichosahaulika
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i38119-bahrain_kisiwa_kilichosahaulika
Mahakama ya Kijeshi ya Bahrain Jumatatu ilitoa hukumu ya kifo dhidi ya wafungwa sita kwa madai kuwa eti walihusika na njama za kutaka kumuua mkuu wa jeshi la Bahrain. Watuhumiwa wengine saba wamehukumiwa kifungo cha miaka saba jela.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 26, 2017 03:52 UTC
  • Bahrain, kisiwa kilichosahaulika

Mahakama ya Kijeshi ya Bahrain Jumatatu ilitoa hukumu ya kifo dhidi ya wafungwa sita kwa madai kuwa eti walihusika na njama za kutaka kumuua mkuu wa jeshi la Bahrain. Watuhumiwa wengine saba wamehukumiwa kifungo cha miaka saba jela.

Zinakaribia siku 50 kabla ya kumalizika mwaka wa saba wa maandamano na malalamiko ya Wabahrain dhidi ya ukoo wa Aal Khalifa unaotawala kiimla nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi. Mwamko wa watu wa Bahrain una nukta kadhaa zanazoufanya uwe wa kipekee na tafauti ikilinganishwa na malalamiko mengine yaliyoshuduiwa katika nchi za Kiarabu kuanzia Februari 14 mwaka 2011.

Tafauti muhimu zaidi ya mwamko wa Bahrain na harakati zalizoshuhudiwa Tunisia, Misri, Libya  na Yemen ni kuwa nchini Bahrain kuna dola la kigeni ambalo limetuma wanajeshi wake nchini humo kwa lengo moja pekee, nalo ni kukandamiza maandamano ya wananchi. Saudia Arabia ambayo inaitazama Bahrain kama moja ya majimbo yake, mwezi mmoja tu baada ya kuanza malalamiko ilitangaza kutuma wanajeshi wake katika nchi hiyo ndogo kwa lengo la kuulinda utawala wa kiimla wa ukoo wa Aal Khalifa na kuzima mapinduzi ya wananchi. Ni kwa msingi huo ndio wanamapinduzi wa Bahrain wakaitaja hatua hiyo ya Saudia kuwa ni kuikalia kwa mabavu nchi yao.

Nukta ya pili ya kipekee ya mwamko wa watu wa Bahrain dhidi ya ukoo wa Aal Khalifa ni kuwa, pamoja na kuwa mwamko huo umekuwa ukiendelea kwa muda mrefu sambamba na ukandamizaji na ukatili unaotumiwa na ukoo wa Aal Khalifa, lakini wananchi wa nchi hiyo katu hawajachukua silaha mikononi mwao na kwa msingi huo maandamano ya wananchi yanafanyika kwa amani. Hii ni katika hali ambayo katika nchi zingine za Kiarabu, maandamano na malalamiko ya wananchi yameshuhudia ghasia na machafuko na hata baadhi ya nchi hizo kama vile Libya na Bahrain zimetumbukia katika vita vya ndani.

Utawala wa Bahrain unatumia nguvu ziada kukabiliana na waandamanaji

Nukta ya tatu ya kipekee ya mwamko wa watu wa Bahrain ni kuwa, kinyume na nchi nne za Misri, Tunisia, Libya na Yemen ambazo zimeshuhudia mabadiliko au kupinduliwa mifumo iliyokuwa ikitawala, nchini Bahrain katika kipindi cha miaka saba hakujashuhudiwa mabadiliko yoyote ya utawala.

Waandamanaji wangali wanaendeleza malalamiko nao utawala wa kiimla wa ukoo wa Aal Khalifa kuendeleza ukandamizaji wake na kilichobadilika tu ni mbinu za ukandamizaji huo.

Moja ya mabadiliko makubwa zaidi katika mbinu za ukandamizaji Bahrain ni kuongezwa hukumu ya kifo au kunyongwa waandamanaji na pia kutumiwa mahakama za kijeshi kusikiliza kesi za kiraia.

Kwa mara ya kwanza katika mwezi Januari mwaka 2017, utawala wa Bahrain ulitoa hukumu ya kifo dhidi ya vijana watatu ambao walituhumiwa kuwa eti mwaka 2014 walihusika katika utegaji wa bomu lililopelekea kuuawa maafisa watatu wa polisi. Hukumu ya kifo dhidi ya vijana hao ilitekelezwa pamoja na kuwepo malalmiko ya taasisi za haki za binadamu. Tukiwa tunakaribia kumbukumbu ya hukumu hiyo ya kidhalimu, utawala wa Aal Khalifa umetoa hukumu ya kunyongwa raia wengine watatu wa nchi hiyo.

Mfalme wa Bahrain akiwa na Waziri Mkuu wa Uingereza, nchi ambayo inaunga mkono ukandamizaji dhidi ya Wabahrain

Pamoja na kuwepo na sifa hizo za kipekee katika mwamko wa wananchi wa Bahrain lakini jamii ya kimataifa hadi sasa haijaulaani utawala wa kiimla wa Aal Khalifa. Hakuna azimio lolote limepasishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili huo unaofanywa na Bahrain dhidi ya raia wake. Kimsingi ni kuwa Umoja wa Mataifa umepuuza kabisa dhulma inayowakabili watu wa Bahrain.

Kama alivyosema Graham Fuller, mtafiti wa masuala ya nchi za Kiislamu, "Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Bahrain wamesahauliwa na sasa tunaweza kusema kuwa Bahrain ni kisiwa kilichosahaulika. Huku ni kushahauliwa ambako kumewapa fursa watawala wa ukoo wa Aal Khalifa kuendelea na jinai zao na hivi sasa sauti ya watu wa Bahrain imekandamizwa."