Ndege za Saudia zaua raia 20 katika hujuma magharibi mwa Yemen
Raia wasiopungua 20 wameuawa katika hujuma ya ndege za kivita za Saudi Arabia dhidi ya makao ya raia katika mkoa wa al Hudaydah magharibi mwa Yemen.
Kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Yemen, Saba, ndege za kivita za Saudia zililenga magari mawili ya kiraia karibu na mgahawa ulio katika wilaya ya al-Jarahi Jumamosi.
Mapema hiyo jana pia ndege za kivita za Saudi Arabia zilishambulia shamba moja magharibi mwa Yemen na kuua wanawake wasiopungua 10 waliokuwa katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa ripoti ya Jumamosi ya televisheni ya Al-Masirah, ndege za kivita za Saudia zilidondosha mabomu katika shamba lililo katika Wilaya ya Khoukha mkoani al-Hudaydah katika ukanda wa pwani wa magharibi mwa nchi hiyo.
Jumanne iliyopita pia ndege za kivita za Saudia zilidondosha mabomu katika soko mkoani Ta'izz kusini magharibi mwa Yemen na kuua makumi ya raia wasio na hatia.
Tangu mwezi Machi mwaka 2015, Saudia, ikisaidiwa na kuungwa mkono na baadhi ya nchi za Kiarabu na Marekani ilianzisha mashambulio ya kinyama dhidi ya Yemen kwa lengo la kutaka kumrejesha madarakani kibaraka wake Abd Rabbuh Mansur Hadi, rais wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kuitoroka nchi.
Hadi sasa watu zaidi ya 13,000, wengi wao wakiwa watoto na wanawake, wameuawa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi kutokana na mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya nchi hiyo.