Kuitetea Palestina ndiko kumefanya maadui wachochee ghasia Iran
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kimataifa ya Wanazuoni Wanamuqawama sambamba na kulaani machafuko yanayoendelea kushuhudiwa katika baadhi ya maeneo hapa nchini Iran, amesisitiza kuwa maadui Wamagharibi ndio waliochochea ghasia hizi kutokana na msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu wa kuitetea Palestina na kuunga mkono harakati za muqawama.
Sheikh Maher Hamoud ameyasema hayo katika mazungumzo ya simu na Ayatullah Mohsen Araki, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu.
Sheikh Hamoud amepongeza hatua ya serikali ya kuwaruhusu wananchi wafanye maandamano ya amani lakini akabainisha kuwa, ghasia ni jambo ambalo halikubaliki.
Ameongeza kuwa, wananchi wa Iran wanapaswa kuunga mkono msimamo wa serikali yao wa kuwatetea Wapalestina mkabala wa njama za maadui wa taifa hili hususan Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Kwa upande wake, Ayatullah Mohsen Araki, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu ya Kiislamu amesema bila shaka matakwa halali wanayoyashinikiza Wairani yatashughulikiwa na kuongeza kuwa, hali ya mambo sio mbaya kama jinsi vyombo vya habari vya Magharibi vinavyojaribu kusawiri.
Amefafanua kuwa, vitendo vya uvunjifu wa sheria vinavyofanywa na baadhi ya waandamanaji vimechochewa na uingiliaji wa masuala ya ndani wa Washington na Tel Aviv.