Maulamaa wa Palestina: Iran inaunga mkono kadhia ya Palestina
Baraza la Maulamaa wa Kiislamu huko Palestina limetangaza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikiunga mkono kwa hali na mali kadhia ya Palestina.
Sheikh Muhammad Salah al-Mauid, msemaji wa Baraza la Maulamaa wa Palestina huko nchini Lebanon ametangaza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni muungaji mkono wa mageuzi na uhuru wa kutoa maoni na kwamba, nchi yenye nguvu ya Iran imekuwa ikilipa gharama za msaada na uungaji mkono wake kwa taifa madhulumu la Palestina.
Mwanazuoni huyo wa Kisuni amebainisha kwamba, vurugu zilizoibuka nchini Iran hivi karibuni ni njama za maadui na kuongeza kuwa, kujitokeza mamilioni ya wananchi wa Iran katika maandamano ya kulaani uungaji mkono wa Marekani na utawala dhalimu wa Israel kwa wazushaji fujo ni ishara ya kufikia tamati njama hizo.
Wakati huo huo chama cha Tawhid al-Arabi cha nchini Lebanon kimeonyesha kusikitishwa kwake na matukio ya hivi karibuni nchini Iran na kusisitiza kwamba, kina uhakika na uwezo wa Iran wa kuzima njama hizo.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, maandamano ya mwamko ya wananchi wa Iran yaliendelea kushuhudiwa tena hapo jana katika kuunga mkono malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu na kulaani vitendo vya kuzusha fujo na uingiliaji wa Marekani na utawala wa Kizayuni katika masuala ya ndani ya Iran.