Mtaalamu: Hizbullah itaibuka mshindi katika vita vyovyote na Israel
Uwezo wa harakati ya Kiislamu ya Hizbullah nchini Lebanon katika nyuga tofauti zikiwemo za kijeshi, vita stadi na vita vya kisaikolojia umeutia kiwewe utawala haramu wa Kizayuni wa Israel kiasi cha kuwafanya weledi wa masuala ya kivita kusema kwamba, vita vyovyote vitakavyojiri kati ya Israel na harakati hiyo, vitamalizika kwa ushindi wa Hizbullah.
Muhammad Ali Jafar, mtaalamu wa masuala ya kistratijia katika mtandao wa habari wa al-Ahdi nchini Lebanon ameandika kwamba, kuongezeka uwezo wa hali ya juu wa harakati hiyo ya Kiislamu sambamba na kuwa na stratijia mpya ni jambo lililozidisha wasi wasi na wahka mkubwa kwa utawala wa Kizayuni.
Kwa mujibu wa Jafar, stratijia hizo zinazotumiwa hivi sasa na Hizbullah zinabadili nukta dhaifu kuwa fursa zenye umuhimu kwa ajili ya kukabiliana na adui. Aidha mtaalamu huyo wa masuala ya kistratijia ameelezea namna ambavyo taswira ya harakati ya Hizbullah inavyoogopesha katika fikra za utawala wa Kizayuni kutokana na uwezo wake mkubwa wa kijeshi. Muhammad Ali Jafar amebainisha kwamba harakati hiyo inaendesha vita kupitia stratijia yenye nguvu na akili na kwa mujibu wa viwango vya kijeshi vya kisasa, licha ya jeshi la Israel kutumia kiwango cha juu cha teknolojia yake, lakini Hizbullah imefanikiwa kugeuza uwezo wa jeshi la utawala huo na kuwa nukta ya udhaifu.
Amezidi kufafanua kuwa, tatizo la Israel halipo kwenye namna ya kukabiliana na uwezo wa makombora ya Hizbullah, bali lipo kwenye uwezo wa kistratijia ambao harakati hiyo inaumiliki kwa sasa. Katika vita vya siku 33 kati ya Israel na wanamuqawama wa Hizbullah vilivyoanza mwezi Julai mwaka 2006 na kumalizika tarehe 14 mwezi Agosti mwaka huo huo, harakati hiyo ya Kiislamu iliibuka mshindi.