UN: Answarullah imefungamana na mazungumzo ya amani
Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Yemen amesema kuwa, harakati ya wananchi ya Answarullah nchini humo imetoa taarifa ya kuheshimu na kufungamana na suala la kuanza upya mazungumzo ya amani nchini humo.
Ismaïl Ould Cheikh Ahmed ameandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter akizitaka pande zote za Yemen kufanya mazungumzo ya maridhiano, ushirikiano, amani, maafikiano na ujirani mwema. Kadhalika mwakilishi huyo wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekaribisha juhudi za Maeen Sharim, msaidizi wake aliyekutana na viongozi wa Yemen mjini Sana'a kwa ajili ya kuanzisha tena mwenendo wa amani mapema zaidi.
Jumatatu iliyopita msaidizi huyo wa Ismaïl Ould Cheikh Ahmed alikutana mjini Sana'a na Saleh Ali al-Sammad, mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen na viongozi wengine wa taifa hilo. Katika mazungumzo hayo al-Sammad alimueleza Sharim kuhusu maandalizi ya serikali ya Yemen kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya pande mbili kwa shabaha kuhitimisha mgogoro wa nchi hiyo na kurejesha usalama na amani nchini.
Mazungu kati ya makundi tofauti ya Yemen yamefanyika mara kadhaa, hata hivyo kutokana na sera za Saudia za kuingilia kati masuala ya ndani ya nchi hiyo, yalimalizika bila kufikiwa makubaliano. Wakati huo huo, jeshi la Yemen kwa kushirikiana na harakati ya wananchi ya Answarullah limetangaza habari ya kuangamizwa makumi ya vibaraka wa Saudia katika maeneo kadhaa ya mkoa wa Al Jawf nchini humo.
Duru ya habari nchini humo imetangaza kwamba, katika operesheni hiyo jeshi la Yemen na harakati hiyo ya wananchi limefanikiwa kudhibiti silaha kutoka kwa vibaraka hao. Hii ni baada ya vibaraka hao kujaribu mara mbili kupenya katika maeneo ya jeshi na harakati ya wananchi ya Answarullah katika maeneo ya al-Shaqab, al-Mafalis na Haifan ya mkoa wa Taiz, kusini mwa Yemen bila mafanikio.