Human Rights Watch: Saudia inakiuka haki za binadamu nchini Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i39159-human_rights_watch_saudia_inakiuka_haki_za_binadamu_nchini_yemen
Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch limetangaza kuwa, Saudi Arabia imekuwa ikikiuka haki za binadamu huko nchini Yemen.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 19, 2018 00:10 UTC
  • Human Rights Watch: Saudia inakiuka haki za binadamu nchini Yemen

Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch limetangaza kuwa, Saudi Arabia imekuwa ikikiuka haki za binadamu huko nchini Yemen.

Ripoti ya Human Rights Watch mbali na kueleza kwamba, Saudia imekuwa ikikiuka haki za binadamu huko nchini Yemen imebainisha pia kuwa, utawala wa Aal Saud umekuwa ukiwatia mbaroni na kuwafunga jela wanaharakati wa kisiasa ambao wamekuwa wakidai kwa amani mageuzi ya kisiasa katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Sarah Leah Whitson, Mkurugenzi wa Human Rights Watch kitengo cha Mashariki ya Kati ametangaza kuwa, kuendelea hali mbaya ya kibinadamu nchini Yemen na wakati huo huo kutiwa mbaroni na kuhukumiwa jela wanaharakati wa kisiasa kwa kubambikiziwa kesi ni mambo ambayo yameharibu haiba ya Muhammad bin Salman mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia.

Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch

Katika miezi ya hivi karibuni wanamfalme wapinzani, wanaharakati wa kisiasa na waandishi wametiwa mbaroni kwa amri ya Muhammad bin Salman. Baadhi ya ripoti zinaonyesha kuwa, kuna wafungwa wa kisiasa wapatao 30,000 katika magereza ya Saudia, takwimu ambazo zinaakisi kushadidi siasa za kipolisi za utawala wa kidikteta wa Aal Saud dhidi ya wananchi wa nchi hiyo.

Huku ndani ya Saudia hali ikiwa hivyo, hatua ya watawala wa Riyadh ya kuendelea kuishambulia kijeshi Yemen imezidi kusababisha maafa makubwa kwa wananchi wa nchi hiyo masikini ya Kiarabu na kupelekea kujitokeza ukosoaji mkubwa katika kila kona ya dunia.