Saeb Erekat: Taifa la Palestina katu halitakubali matakwa ya Marekani
Katibu wa kamati ya utendaji ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) amesema kuwa, matakwa na siasa za kuegemea upande mmoja za Marekani zinazotekelezwa kwa maslahi ya utawala haramu wa Israel katu hazikubaliwi na taifa la Palestina.
Saeb Erakat amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na Televisheni ya al-Jazeera ya Qatar na kusisitiza kwamba, taifa madhulumu la Palestina katu halitasalimu amri mbele ya matakwa ya Marekani na washirika wake.
Akijibu kauli ya Mike Pence, Makamu wa Rais wa Marekani kwamba, yuko tayari kufanya mazungumzo na kushirikiana na Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Katibu wa Kamati ya Utendaji ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) amesema bayana kwamba, mazungumzo ya aina yoyote ile na Marekani hasa baada ya hatua ya Rais Donald Trump ya kuitangaza Beitul-Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala ghasibu wa Israel haitakuwa hatua ya kimantiki.
Erakat amesema kuwa, madai ya Wamarekani kwamba, kutohudhuria Wapalestina kwenye mazungumzo ya mapatano kunakwamisha mwenendo wa amani ni ya kichekesho.
Amesema, Makamu wa Rais wa Marekani amewatuhumu Wapalestina kwamba, walikwamisha mazungumzo 2014, katika hali ambayo, hatua ya Benjamin Netanyahu ya kuendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni ndio iliyokwamisha mazungumzo hayo.
Katibu wa kamati ya utendaji ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) amesisitiza kwamba, madhali Marekani inafuatilia kuyatokomeza mafaili ya Quds na wakimbizi wa Kipalestina, taifa la Palestina katu haliwezi kufanya muamala wowote ule na serikali ya Washington.