Umoja wa Mataifa watakiwa kuchunguza mauaji yanayofanywa dhidi ya Wapalestina
Mamlaka ya Ndani ya Palestina imeutaka Umoja wa Mataifa kufanya uchunguzi kuhusu mauaji ya kidhalimu yanayofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina.
Wito huo umetolewa baada ya askari wa Israel kufanya jinai ya kumpiga risasi na kumuua kijana majeruhi wa Kipalestina, Abdul Fattah Sharif aliyekuwa na umri wa miama 21 katika eneo la Ukingo wa Magharibi.
Mauaji hayo ya Mpalestina aliyekuwa amejeruhiwa yamelaaniwa sana katika duru mbalimbali za kimataifa na vilevile jumuiya mbalimbali za kutetea haki za binadamu.
Baada ya kukabiliwa na wimbi kubwa la malamiko, utawala wa Kizayuni umedai kuwa askari aliyempiga risasi kichwa na kumuua kijana huyo aliyekuwa amejeruhiwa amekamatwa na kwamba umeanza uchunguzi kuhusu jinai hiyo.
Zaidi ya raia 200 wa Palestina wameuawa kwa kupigwa risasi na askari wa Israel tangu kuanza kwa mapambano ya Intifadha ya Quds mwanzoni mwa mwezi Oktoba mwaka jana. Maelfu ya wengine wamejeruhiwa.