Israel yawauawa shahidi Wapalestina wawili, Hamas yajibu
Vijana wawili wa Kipalestina wameuawa shahidi kufuatia mashambulizi ya jeshi la utawala katili la Israel katika Ukanda wa Gaza.
Wizara ya Afya ya Palestina imewatambua vijana hao kwa majina ya Salam Sabah na Abdullah Abu Sheikha, wote wawili wana umri wa miaka 17.
Mashuhuda wanasema vijana hao waliuawa jana Jumamosi katika mji wa Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza, baada ya jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel kuanzisha mashambulizi ya anga na ya roketi dhidi ya eti ngome za harakati ya Muqawama ya Palestina Hamas.
Wakati huo huo, wanamapambano wa Izzuddin Qassam, tawi la kijeshi la Hamas wametangaza habari ya kutumia mfumo wao wa ulinzi dhidi ya mashambulizi hayo ya anga ya Israel, sambamba na kuanzisha mashambulizi ya kulipiza kisasi.
Jeshi la Israel limekiri kuwa roketi lililovurumishwa kutoka eneo la Gaza limedondoka juu ya paa la nyumba katika mji mmoja wa utawala huo ghasibu.
Wapalestina wasiopungua 148 walijeruhiwa Ijumaa iliyopita wakati wakikabiliana na wanajeshi wa Utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza.