Mahakama Bahraini yaidhinisha hukumu ya kifo kwa mpinzani wa utawala
Mahakama ya kilele ya rufaa nchini Bahraini imeidhinisha hukumu ya kifo iliyotolewa dhidi ya mwanaharakati wa Kishia ambaye amekuwa akiupinga utawala wa kiimla wa ukoo wa Aal Khalifa katika nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi.
Katika hukumu hiyo ya jumatatu, mahakama imedai kuwa Hussein Marzouq alihusika na ulipuaji bomu mwaka 2016 katika kijiji cha Sitra yapata kilomita tano kutoka mji mkuu Manama. Imedaiwa kuwa hujuma hiyo ilikuwa imelenga maafisa wa kijeshi wa utawala wa kifalme. Mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo amehukumiwa kifungo cha maisha jela huku wengine sita wakifungwa vifungo vya muda mrefu mbali na kupokonywa uraia.
Hayo yanajiri huku utawala wa Bahrain ukiendelea kutumia mkono wa chuma kukandamiza maandamano ya amani ya wapinzani wanaopinga ubaguzi na udhalilishwaji wanotendewa waliowengi nchini humo ambao ni Waislamu wa madhehebu ya Shia.
Ikumbukwe kuwa, Bahrain imekuwa ikishuhudia maandamano ya amani ya wananchi wanaopinga utawala wa Aal Khalifa tangu Februari mwaka 2011. Matakwa makuu ya wananchi hao ni kuwepo utawala wa kisheria, kukomeshwa ubaguzi wa kimadhehebu, utawala wa demokrasia na kuheshimiwa haki za binadamu.