Wanaharakati 116 wanaopinga ufalme wakamatwa Bahrain
Maafisa wa polisi nchini Bahrain wamewakamata wanaharakati 116 wanaopinga ufalme wa ukoo wa Aal Khalifa huku ukandamizaji wa wapinzani ukiendelea kushika kasi katika nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi.
Taarifa ya shirika rasmi la habari la Bahrain BNA, imedai kuwa wanaharakati hao ni wanachama wa eti kundi la 'kigaidi' na kwamba eti walipanga kufanya hujuma katika nchi hiyo.
Taarifa hiyo imedai kuwa eti waliokamatwa wanahusiana na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu Iran. Hata hivyo kwa mara kadhaa sasa Iran imekuwa ikikanusha kuhusika na mikakati yoyote ya kutaka kuupindua utawala wa Bahrain.
Inafaa kuashiria kuwa harakati za mapinduzi ya amani ya wananchi nchini Bahrain zilianza Februari 14 mwaka 2011. Ni miaka saba sasa imepita tangu wananchi wa nchi hiyio walipoanzisha maandamano ya amani wakitaka kunfayike marekebisho ya kisiasa sambamba na kukomeshwa ubaguzi dhidi ya Waislamu wa Kishia ambao ndio walio wengi nchini Bahrain.
Hata hivyo badala ya utawala wa Aal Khalifa kusikiliza malalamiko ya wananchi, unatumia ukandamizaji wa kuchupa mipaka sambamba na kuomba masaada zaidi wa askari vamizi wa Saudia walioingia nchini humo na kufanya jinai nyingi dhidi ya binaadamu.