Mahakama Misri yaidhinisha Saudia kupewa visiwa vya nchi hiyo
Mahakama ya Juu nchini Misri imefutilia mbali maamuzi yaliyotolewa na mahakama za chini za nchi hiyo kuhusu mpango wa kukabidhi visiwa viwili vya kistratajia vya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika kwa Saudi Arabia.
Katika hukumu iliyotolewa hapo jana, Mahakama ya Juu ya Misri imebatilisha hukumu zote zilizotolewa huko nyuma na mahakama za chini, kuhusiana na mpango huo wa kukabidhiwa Riyadh visiwa vya Tiran na Sanafir, ambao ulizusha ghadhabu, malalamiko na maandamano nchini humo.
Hukumu hiyo yenye utata imetolewa masaa machache kabla ya kuwasili nchini humo leo Jumapili, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia, Mohammad Bin Salman, kwa ajili ya kufanya safari ya siku tatu.
Mapema mwezi uliopita, duru za habari nchini humo ziliarifu kwamba, Saudia tayari imetwaa kwa siri kisiwa cha Tiran kilichopo Bahari Nyekundu.
Rais Abdel Fattah el-Sisi wa Misri na katika kuboresha mahusiano kati ya Cairo na Riyadh aliamua kuiuzia Saudia visiwa vya Tiran na Sanafir mwaka 2016, hatua ambayo ilikabiliwa na malalamiko makubwa ya Wamisri.
Mazungumzo yaliyovuja ya simu yanaonyesha kuwa Misri iliwasiliana na utawala wa Kizayuni wa Israel ili kupata baraka na uungaji mkono wake kabla ya kusaini muafaka wa mauziano hayo.