Hamas yasisitiza kukombolewa Palestina
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imesema kuwa mapambano ndio njia pekee ya kukomboa ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni wa Isarel.
Taarifa iliyotolewa na harakati ya Hamas imesema kwa mnasaba wa Siku ya Ardhi kuwa, mapambano dhidi ya adui Mzayuni ndio chaguo la kistratijia la taifa la Palestina kwa ajili ya kurejesha haki zake, kulinda thamani na matukufu yake na kukomboa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.
Hamas imelaani njama zinazofanywa na adui za kutaka kubadili na kufuta kabisa alama, athari na matukufu ya Kiislamu na kusisitiza kuwa, taifa la Palestina litaendeleza mapambano ya kupigania haki zake dhidi ya Wazayuni maghasibu.
Harakati ya Hamas pia imezitaka nchi za Kiarabu na Kiislamu kutekeleza majukumu yao ya kulinda matukufu ya Palestina mbele ya hatari na mashambulizi ya Wazayuni maghasibu.
Wapalestina wanaoishi katika ardhi zilizoghusubiwa na Israel mwaka 1948 huadhimisha tarehe 30 Machi kila mwaka kama Siku ya Ardhi ambayo inakumbusha tukio chungu la mwaka 1976 ambapo Israel ilitwaa ardhi kubwa ya maeneo ya al Jalil.