Al Abadi: Ugaidi umemalizika kijeshi Iraq, sasa ni vita vya kifikra
Waziri Mkuu wa Iraq amesema kwa mtazamo wa kijeshi, ugaidi umeshindwa na kumalizika nchini Iraq na sasa hatua inayofuata ni kukabiliana na fikra za kigaidi.
Haidar al Abadi Waziri Mkuu wa Iraq ameyasema hayo leo mjini Baghdad katika maonyesho ya usalama na ulinzi na kuongeza kuwa: "Leo silaha ambazo Iraq inamiliki si za kutekeleza hujuma za kijeshi bali ni kwa ajili ya kufikia amani na ujenzi mpya wa nchi ".
Al Abadi aidha amesema, dikri aliyosaini ya kuingiza vikosi vya kujitolea vya wananchi, Al-Hashd Al-Shaabi, katika vikosi vya usalama vya Iraq ni kwa lengo la kuwaunga mkono wananchi wa Iraq.
Siku ya Alhamisi, Al Abadi alitia saini dikrii rasmi ya kujumuishwa Al-Hashd Al-Shaabi katika vikosi vya usalama vya Iraq.
Wakati huo huo wapiganaji wa Al-Hashd Al-Shaabi wa Iraq wamevurumisha makombora na kuwalenga magaidi kaskazini mwa Syria. Taarifa ya kikosi hicho imesema magaidi wa ISIS walikuwa wamejumuika katika kijiji cha Al Atwashana katika ardhi ya Syria kwa lengo la kushambulia wanajeshi wa Iraq katika ukanda wa mpakani.
Magaidi hao wamekuwa katika kijiji hicho tokea Februari 2018 na wamelengwa mara kadhaa na wapiganaji wa Al-Hashd Al-Shaabi ambao wako katika eneo la mpaka wa Iraq na Syria.