Wimbi jipya la malalamiko ya wananchi nchini Bahrain
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i41853-wimbi_jipya_la_malalamiko_ya_wananchi_nchini_bahrain
Jumamosi usiku raia wa Bahrain walifanya maandamano katika maeneo mengi ya nchi hiyo sambamba na kulaani hatua hasi za utawala wa Aal Khalifa kuwalenga wapinzani.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Mar 18, 2018 23:46 UTC
  • Wimbi jipya la malalamiko ya wananchi nchini Bahrain

Jumamosi usiku raia wa Bahrain walifanya maandamano katika maeneo mengi ya nchi hiyo sambamba na kulaani hatua hasi za utawala wa Aal Khalifa kuwalenga wapinzani.

Jumuiya ya Kiislamu ya Al-Wefaq siku hiyohiyo pia ilitangaza kwamba, tangu kuanza mwaka huu wa 2018 Miladia hadi sasa kumefanyika maelfu ya maandamano ya wananchi katika maeneo mengi ya nchi hiyo. Wimbi jipya na harakati mbalimbali za malalamiko ya Wabahrain dhidi ya serikali zinajiri licha ya ukandamizaji na kamatakamata iliyoshtadi sambamba na kujizuia vyombo vya habari vya utawala wa Aal-Khalifa kuakisi matukio hayo. Matukio ya Bahrain katika miaka kadhaa iliyopita, yanabainisha kwamba muqawama wa raia wa nchi hiyo ni jambo lisiloweza kuzimwa na badala yake kila siku muqawama huo unazidi kuongezeka.

Maandamano ya wananchi

Tangu mwaka 2014 Februari 2011, Bahrain imekuwa ikishuhudia mwamko wa wananchi dhidi ya utawala wa kiimla na kidikteta wa Aal-Khalifa. Katika uwanja huo, Wabahrain wanadai uhuru, kuimarishwa uadilifu, kuondolewa ubaguzi na kuingia madarakani utawala uliochaguliwa na wananchi. Hata hivyo utawala wa Aal-Khalifa badala ya kujibu malalamiko hayo ya wananchi, umeamua kutumia ukandamizaji wa kutisha kuzima malalamiko hayo. Kuhodhi madaraka na utajiri wa nchi, ukoo mmoja na kadhalika raia kuwekewa vikwazo na mibinyo na utawala wa Manama, ni moja ya masuala muhimu na ya msingi yaliyowafanya Wabahrain waamue kupeleka malalamiko yao barabarani tarehe 14 Februari 2011.

Maandamano ya Wabahrain yakiendelea

Hatua za ukandamizaji wa utawala wa Aal-Khalifa si tu kwamba zimeshindwa kusambaratisha mwamko wa wananchi, bali zimesababisha pia kushtadi malalamiko yao siku hadi siku. Harakati ya wananchi wa Bahrain kwa ajili ya kufikia malengo yao halali ya kisiasa, hadi sasa ingali inaendelea ambapo sambamba na kufanya maandamano mtawalia, inataka kutekelezwa matakwa yao. Kuongezeka harakati za malalamiko ya amani ya wananchi mkabala wa ukandamizaji wa utawala wa Aal-Khalifa, kumeufanya utawala huo kuchanganyikiwa na kushindwa kufikia lengo lake la kusimamisha mwamko wa wananchi hao. Katika uwanja huo, mtandao wa habari wa al-Akhbar, umemnukuu mwandishi Hassan Qambar akisema:

Jumuiya ya Al-Wefaq ya Bahrain

"Kwa kuzingatia matukio ya huko nyuma, hivi sasa utawala wa kifalme wa Bahrain ambao umeamua kufuata siasa za mkono wa chuma, umeshindwa kukabiliana na wimbi la malalamiko ya raia. Ripoti hiyo inaendelea kusema kuwa, utawala wa Aal Khalifa ulidhania kwamba kwa kutumia ukandamizaji na vitisho, kukiwemo kutegemea msaada wa askari wa Saudia, ungeweza kuzima moto wa mwamko wa wananchi, lakini kinyume na matarajio ya mfalme na ukoo wa Aal Khalifa, sambamba na kupita muda mrefu wa maandamano hayo umebaini kwamba kadri unavyoongeza ukandamizaji, ndivyo msimamo wa wananchi wa kutaka marekebisho na mabadiliko nchini mwao, unavyozidi kushika kasi. Katika mazingira hayo, wapinzani wa Bahrain wangali wanaendeleza maandamano yao, ambapo mwaka 2018 wamepiga nara wakisema, 'Sisi tumesimama kwa irada yenye nguvu.' Mwisho wa kunukuu.

Mtandao wa al-Akhbar

Kuendelea maandamano ya wananchi dhidi ya utawala wa Manama mwaka huu, kunabainisha kuongezeka azma yao thabiti katika kufuatilia malengo ya mwamko wao dhidi ya utawala huo wa kidikteta. Aidha raia wa Bahrain licha ya mashinikizo na ukandamizaji mkubwa dhidi yao, bado wanaendelea kusisitizia udharura wa kutekelezwa matakwa yao halali. Kuendelea mwamko wa wananchi nchini Bahrain pamoja na mambo mengine, kunabainisha ni kwa kiasi gani utawala wa Aal Khalifa unakabiliwa na mgogoro mkubwa wa ndani.