Wapinzani 32 wakamatwa Bahrain masaa 24 yaliyopita
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i42094-wapinzani_32_wakamatwa_bahrain_masaa_24_yaliyopita
Utawala wa kiimla wa Bahrain umewakamata wapinzani 32 katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita huku ukandamizaji ukiendelea kushika kasi nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 24, 2018 02:48 UTC
  • Wapinzani 32 wakamatwa Bahrain masaa 24 yaliyopita

Utawala wa kiimla wa Bahrain umewakamata wapinzani 32 katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita huku ukandamizaji ukiendelea kushika kasi nchini humo.

Taarifa zinasema askari wa utawala wa Aal Khalifa walihujumu kijiji cha Diraz kilicho kilomita 12 kutoka mji mkuu Manama na kuwakamata watu kadhaa wanaoupinga ufalme, wakiwemo watoto wadogo. Aidha maafisa wa usalama walihujumu kijiji cha Buri kilicho kilomita 13 kusini magharibi mwa Manama na kuwakamata ndugu wawili, Abdullah na Mohammed Saleh Mahdi.

Kijiji cha Diraz ni mahali yalipo makazi ya Sheikh Issa Qassim, mwanazuoni mashuhuri nchini Bahrain ambaye tokea Juni 2016 amekuwa katika kizuizi cha nyumbani alichowekewa na utawala wa kiimla wa Aal Khalifa.

Maandamano ya kupinga utawala wa kiimla Bahrain

Tarehe 14 Februari mwaka 2011 wananchi wa Bahrain walianzisha vuguvugu la mapambano kwa kufanya maandamano ya amani dhidi ya utawala wa Aal Khalifa. Hata hivyo utawala huo, unaopata himaya ya Marekani na Saudi Arabia,sio tu umeamua kutumia mkono wa chuma kuyakandamiza mapambano ya Wabahraini lakini pia umekuwa ukichukua hatua kali dhidi ya viongozi wa kidini na kisiasa ili kuhakikisha mapambano hayo hayaendelezwi kwa kufuata miongozo ya viongozi hao.