Iraq: Saudia ituombe radhi kwa kutuma magaidi elfu 5 nchini
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i42164-iraq_saudia_ituombe_radhi_kwa_kutuma_magaidi_elfu_5_nchini
Muungano wa Utawala wa Sheria nchini Iraq umeutaka utawala wa Aal-Saud wa Saudi Arabia uliombe radhi taifa hilo kutokana na madhara lililoyapata, kwa hatua ya Riyadh kutuma maelfu ya magaidi katika nchi hiyo ya Kiarabu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 25, 2018 06:18 UTC
  • Nouri al Maliki, Waziri Mkuu wa zamani wa Iraq
    Nouri al Maliki, Waziri Mkuu wa zamani wa Iraq

Muungano wa Utawala wa Sheria nchini Iraq umeutaka utawala wa Aal-Saud wa Saudi Arabia uliombe radhi taifa hilo kutokana na madhara lililoyapata, kwa hatua ya Riyadh kutuma maelfu ya magaidi katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Muungano huo unaoongozwa na Waziri Mkuu wa zamani wa Iraq, Nouri al-Maliki umesema wakati umefika kwa Riyadh kuiomba radhi Baghdad kwa kuiingiza nchi hiyo katika matatizo ya ugaidi kwa miaka kadhaa.

Katika mahojiano na televisheni ya al-Sumariya, Abbas al-Mousawi, msemaji wa Muungano wa Utawala wa Sheria nchini Iraq ametilia shaka mkondo wa kidiplomasia unaotumiwa na Saudia wa kusuluhisha mkwaruzano huo, kwa kutuma timu yake ya taifa ya soka nchini humo ikacheze mchuano wa kirafiki na Iraq, katika hali ambayo hadi sasa Saudia haijajitokeza na kuwaomba radhi rasmi wananchi wa Iraq.

Magaidi wa Daesh (ISIS) waliosambaratishwa nchini Iraq

 

Amesema watawala wa Aal-Saud wanapaswa kwanza kabisa kuweka wazi msimamo wao kuhusu ugaidi, na kisha kuliomba radhi taifa la Iraq kutokana na maneno makali yaliyotolewa na wanazuoni wa Saudia dhidi ya mchakato wa kisiasa wa Iraq.

Julai mwaka jana, Ali Jaber al-Tamimi, mchanganuzi wa kisiasa nchini Iraq alisema Saudia mbali na kuiomba radhi Iraq kwa kuunga mkono harakati za kigaidi dhidi yake, inapaswa pia kuwafungulia mashtaka wanazuoni wake 40, ambao walitoa fatua ya kuhalalisha kuuawa Waislamu wa madhehenu ya Shia nchini Iraq. 

Itakumbukwa kuwa, tarehe 9 Disemba mwaka jana 2017, Iraq ilitangaza rasmi kukombolewa kikamilifu ardhi za nchi hiyo zilizokuwa zinakaliwa kwa mabavu na magaidi wa Daesh na kusisitiza kuwa huo ni ushindi wa kihistoria kwa taifa hilo la Kiarabu.